May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Serikali inatengeneza mazingira wezeshi’

Exaud Kigahe Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa sekta binafsi ili iweze kuanzisha na kuendeleza shughuli za viwanda nchini. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 10 Mei 2021, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mheza mkoani Tanga, Hamis Mwinjuma (Mwana FA).

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa, kumejengwa kiwanda cha kuchakata viungo wilayani Mheza?” Mwinjuma aliuliza.

Akijibu swali hilo, Kigahe amesema serikali inatambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa uchumi, hivyo imeendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa sekta binafsi ili kuanzisha na kuundeleza shughuli za viwanda nchini.

Amesema, wizara kupitia shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO), inaendelea kutoa huduma mbalimbali zinazohusiana na uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati.

“Wilaya ya Muheza ina viwanda vidogo vitatu kwa ajili ya kuchakata viungo, vinavyofanya kazi ni viwili ambavyo ni Trianon Investment Ltd kilichopo Lusanga Muheza mjini ambacho mwaka 2020 kimeuza nje viungo jumla tani 120.

“… na kingine ni G.F.P Organic Ltd kilichopo barabara ya kuelekea Pangani, ambacho mwaka 2020 kiliuza nje jumla ya tani 80 na vibarua zaidi ya 50,” amesema Kigahe.

Kigahe amesema, viungo vinavyochakatwa ni pamoja na Iliki, Mdalasini, Pilipili manga, Karafuu, Mchaichai, Binzari, Maganda ya Machugwa na Limao, aidha kiwanda cha Raza Agriculture Ltd kilichopo katika Kijiji cha Muungano, Muheza vijijini kinatarajia kuanza uzalishaji hivi karibuni.

Amesema, pamoja na viwanda hivyo wilayani Muheza kuna wajasiriamali wadogo wengi ambao husindika viungo katika ngazi ya kaya (household level).

“Hivyo serikali kupitia shirika la viwanda vidogo (SIDO), shirika la viwango Tanzania (TBS) na mamlaka ya biashara Tanzania (TANTRADE) ina wasaidia wajasiliamali hao kwa kuwapatia mafunzo na ushauri ili waweze kuzalisha kwa ubora.

“Napenda kuwaomba wabunge wote kushirikiana na serikali katika kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza zaidi ujenzi wa viwanda vya kuchakata viungo nchini ikiwa ni pamoja na wilaya ya Muheza,” amesema Kigahe.

error: Content is protected !!