Friday , 24 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali inataka kusimamisha au kusimamia dini?
Habari za SiasaTangulizi

Serikali inataka kusimamisha au kusimamia dini?

Rais Magufuli na Viongozi wa Dini
Spread the love

SERIKALI ya Rais John Magufuli, imewasilisha bungeni, muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali – The Written Laws Miscellaneous Amendments No.3 ya mwaka 2019 – ambako pamoja na mengine, kunalengwa kubadilishwa kwa sheria ya vyama vya kijamii. Anaripoti Saed Kubenea … (endelea).

Muswada huu, unaobadili sheria nyingine saba, umeingizwa bungeni kwa njia ya “hati ya dharura.” Swali la kujiuliza, ni hili: Je, kwa nini serikali imeleta muswada huu sasa na kwa hati ya dharura? Kipi kilichomo katika muswada huu na kinalenga nini? Tujadili:  

Kwanza, kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Kijamii (NGO’S), mashirika ya kijamii, ni pamoja na asasi za kidini kama makanisa, taasisi za dini kama Mabohora, Jumuiya za Kiislamu na nyinginezo.

Vyama na mashirika yote haya, husajiliwa chini ya Msajili wa vyama vya Kijamii, wizara ya mambo ya ndani. Baadhi ya mashirika na taasisi hizo, zimekuwapo nchini kabla ya serikali ya kikoloni.

Lakini muswada huu – ikiwa utapitishwa na Bunge na kuwa sheria – unaweza kuzikuta dini zetu hizo, ifikapo tarehe 30 Agosti 2019, zinaweza kujikuta zimefutwa!

Kwamba, viongozi wa taasisi na madhehebu ya kidini, sasa watalazimika kukimbilia kwa waziri wa mambo ya ndani kuomba uhakika wa kuendelea kuwepo. Wasipotimiza masharti ya mapendenkezo ya sheria hii, bila hata kuandikiwa barua na msajili wa vyama vya kijamii, wanakuwa wamejifuta kisheria.

Yani Kanisa Katoliki, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata); Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana; Kanisa la Moravian; Wasabato, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC); Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT); Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste (FPCT) na Shura ya Maimamu, vyote hivyo, vitakuwa vimezimika, mithili ya moto uliyomwagiwa maji.

Hatari kubwa zaidi, ni pale itapotokea akawapo waziri wa mambo ya ndani aliyeugua akili ghafla, akatangaza mahubiri yaliyotolewa na Imamu wa Msikiti wa Kondo, pale Kunduchi, au Msikiti wa Mtambani; ama Kanisa la Forodhani, kwamba yanahatarisha utawala bora, kama ilivyotokea kwa Masheikh wa Jumuiya ya UAMSHO, basi dini nzima inaweza kuadhibiwa!

Kwamba, Msajili na Waziri wake, watakuwa na mamlaka makubwa kuliko Mufti anayesimamia Waislamu takribani 20 milioni – mara mbili ya kura za urais – Askofu, Padri na Mchungaji.

Kwa maneno mengine, mabadiliko haya ya sheria, yanataka kuyafanya makanisa na madhehebu mengine ya kidini, kuwajibika zaidi kwa waziri mteuliwa, kuliko hata waumini, maaskofu na Baba Mtakatifu.

Pili, muswada huu unakuja bungeni, kabla ya joto la barua ya katibu mkuu wizara ya mambo ya ndani, inayoelekeza taasisi za Kidini na Jumuiya za Kijamii, kuhakikiwa kati ya Mei 20 hadi 30 mwaka huu, likiwa bado halijapoa.

Katika barua yake ya tarehe 13 Mei mwaka huu, katibu mkuu wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali, Jacob Kingu, ametaka taasisi hizo kuhakikiwa katika kipindi kilichopangwa. Anasema, wale watakaoshindwa kufanya hivyo, watafutwa kwenye orodha vyama vilivyosajiliwa.

Aidha, muswada unataka taasisi za kidini na mashirika ya kijamii, kuomba ridhaa ya kuendelea kuwepo kwa msajili wa mashirika hayoi. Sheria inasema katika Ibara ya 36 (4), “…yeyote asiyezingatia masharti ya usajili kwa mujibu wa sheria hiyo, atakuwa amefutika ndani ya kipindi cha miezi miwili, tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.”

Vilevile, kuletwa kwa sheria hii, kunaweza kuwa ni kutimia kwa maono ya maaskofu nchini waliyoainisha kwenye waraka wao wa Pasaka mwaka 2018.

Miongoni mwa waliotoa waraka huo, ni Jumuiya ya Kikristo Tanzania na ulisisitiza, “kuwapo kwa hatari ya kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari nchini.”

Kanisa lilisema, “kwa mwenendo huu, kuna hofu ya hata uhuru wa kuabudu, nao kuwa mashakani.”

Kwa mapendekezo haya ya mabadiliko ya sheria, uhuru wa kuabudu sasa utakuwa himaya ya waziri wa mambo ya ndani ama yeyote atakayehusika na kusimamia idara hiyo. Kwamba, kwa sheria hii, taasisi zitalazimika kuomba ridhaa ya waziri ili mahubiri yao “yasije kutishia utawala bora.”

Yaani, waraka waliotoa Maaskofu ama ule wa Baraza Kuu la Taasisi za Kiislamu, ungepaswa kwanza kupata ithibati ya waziri ili kutoiweka dini hatiani.

Swali la kujiuliza: Ni lini serikali imekuwa na dini? Au sasa, serikali ya Rais Magufuli, imeamua kuwa na dini? Je, waziri huyu atateuliwa kati ya makuhani? Atateuliwa na Papa? Atateuliwa na Muunganiko wa viongozi wa dini zote nchini?

Kama siyo hivyo, kwa nini serikali haioni kwamba kujiingiza katika jambo hili la kuzuia watu kuabudu bila ukomo, kutaweza kuharibu au kuchafua amani ya nchi?

Ni vema serikali, ikatambua kuwa sekta binafsi na mashirika ya kidini, ni wadau wa maendeleo. Siyo washindani wa serikali. Kuwatengenezea vikwazo wadau hawa, kutasababisha kukosekana kuaminiana kati ya serikali na sekta hizo.

Hii ni kwa sababu, baadhi ya madhehebu ya kidini, yanaendesha shule za msingi na sekondari, vyuo vikuu na hospitali za wilaya (DDH) na rufaa.

Kwa msingi huo, serikali na Bunge wasipokuwa makini katika kushughulikia muswada huo, hazina hizi zilizojengwa na kutumia mabilioni ya shilingi ya wananchi na wafadhili, zinaweza kutoweka, jambo ambalo litaingiza nchi kwenye mgogoro mkubwa. Tusikubali kufikishwa huko.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Biteko awataka makatibu mahsusi kujiendeleza, kuwa kielelezi cha huduma bora

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 63 ya Uhuru bila katiba ya wananchi

Spread the loveWAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Serikali mbili ni sera ya CCM, si mkataba wa Muungano

Spread the loveMUUNGANO kati ya Tanganyika na Zanzibar uliotimiza miaka 60 tangu...

error: Content is protected !!