Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Serikali imebeba dhambi ya milele
Makala & UchambuziTangulizi

Serikali imebeba dhambi ya milele

Spread the love

WACHINA walilia hata kufikia hatua ya kukufuru kuwa aliyeaga dunia ni mungu wao. Walikuwa wakiomboleza msiba wa muasisi wa taifa lao, Mao Tse Tung Septemba 1976. Anaandika Faki Sosi…(endelea).

Lakini alipohutubia taifa kuhusu msiba huo, mrithi wake, Hua Goufeng, alisema machozi ya Wachina yatakuwa na maana iwapo mawazo ya Mao yatageuzwa ili kukidhi hali halisi ya harakati za maendeleo duniani.

Goufeng hakuishia na kauli, vitendo vyake viliakisi kile alichowaeleza viongozi wenzake na matokeo ya fikra hizo yalishuka moja kwa moja kwa raia.

Viongozi waliona nafasi ya ukomunisti inamezwa na ubepari uchwara ambao mataifa makubwa yanaufanya kuongoza mfumo wa uchumi na siasa duniani.

Viongozi wa China waliamua kuyatumia mawazo ya muasisi wao ili kuingia kwenye sera za kibepari uliopangika vyema, leo hii Wachina wanatembea kifua mbele.

Ni kwa kuwa mawazo ya Mao yalisimamiwa na viongozi waliokuwa na dhamira ya kweli.

Siri kubwa ya China kufikia mapinduzi hayo ni kulinda viwanda, mashamba na migodi iliyokuwa chini ya umiliki wa umma wakati wa utekelezaji wa siasa za ukomunisti ambayo haikubinafsishwa kwa wageni.

Kwanza walianza kujenga uwezo kwa kuwaandaa ‘mabepari’ wa Kichina na kuwauzia viwanda, malighafi na rasilimali nyinginezo, baadaye ndio wakaruhusu wageni kuwekeza wakishindana na ‘mabepari’ wazawa.

Leo hii, ili kumudu ushindani wa ndani, mabepari wageni wanapaswa kujipanga kwelikweli.

Wakati Goufeng akisimamia mawazo ya “Mungu wao” Mao kwa vitendo, Tanzania hawakuweza kuenzi fikra sahihi za muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere uchumi kumilikiwa na dola.

China haikujipamba na fikra alizokuwa nazo Benjamin Mkapa wakati akiwa rais, ambaye baada ya kuingia madarakani aliasisi sera ya kuuza na au kubinafsisha mashirika ya umma.

Kwa bahati mbaya, baadhi yao yalitolewa kwa Watanzania wazawa ambao nao hawakuandaliwa na serikali kumiliki uchumi wao.

Hapa ndipo ilipo tofauti ya Tanzania na China katika ubinafsishaji. Badala ya viongozi kuenzi fikra za Mwalimu Nyerere za uchumi kumilikiwa na dola, walitumia ubinafsishaji kujinufaisha binafsi.

Kutokana na hili serikali inabeba dhambi ya maisha yanayoumiza Watanzania kutokana na kushindwa kuliandaa taifa katika mabadiliko ya kifikra kuhusu dola kumiliki uchumi wake. Harakati za sasa zingekuwa rahisi mno.

Msingi wa maisha haya ni matokeo ya Watanzania kutoandaliwa mapema kuwa wabia wakuu katika uchumi wa taifa lao.

Wakati serikali haijaanza kuchimba madini, gesi, na kuuza magogo nje ya nchi, ilikuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi wake panadol, aspirini, dawa za vidonda, elimu bila gharama yoyote.

Kutokana na kutokuwa na mipango endelevu, baada ya serikali kuanza uchimbaji wa madini yenye thamani kubwa ikiwemo Dhahabu, Almasi, Tanzanite, Kopa, Rubi pia uuzaji wa bidhaa za misitu nje, huduma bila ikawa mwiko. Baado taabu ya maisha imewaganda Watanzania.

Kwa miaka yote serikali ya CCM imekuwa ikitafuta majibu au ufumbuzi wa maisha duni ya Watanzania.

Ni muhimu kujitathmini kwamba, katika harakati zote za kupiga vita umasikini zinazofanywa na serikali, kwanini Watanzania wanaishi maisha ya kulalama? Wengi wao wamekata tamaa.

Hoja ya tuhuma za ufisadi kwa viongozi imeelekezwa katika umiliki wa mali na biashara uliofanywa kwa kificho na baadhi ya viongozi wenyewe au familia zao toka miaka ya nyuma.

Turudie mantiki ya tofauti iliyopo ya China na Tanzania katika ubinafsishaji kwa kutoa mfano. Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira mkoani Mbeya uliishia mikononi mwa mjanja mmoja wakati China wao waliwawezesha wazawa kumiliki uchumi.

Hoja hapa si dhambia kwa viongozi kuanzisha shughuli za kiuchumi lakini yapaswa kuwa mazingira ya wazi na kufuata taratibu.

Hasa baada ya ruksa ya Azimio la Zanzibar mwaka 1992 lililoruhusu viongozi kutoka Rais hadi Mwenyekiti wa Kitongoji kufanya shughuli za kiuchumi kama kilimo ufugaji, uvuvi, biashara, umiliki wa migodi, viwanda, hisa katika kampuni na uanachama wa asasi zisizo za kiserikali.

Ni kwa kuwa hata wakati wa Mwalimu Nyerere mazingira ya wakati wake, aliendesha shughuli za kilimo akiwa Ikulu.

Na hapa ndio maana Rais Jakaya Kikwete alishindwa kufikia dhamira yake ya kutenganisha siasa na biashara.

Lakini pia Mwalimu hakunyonya nguvu za wananchi kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinamlundikia mabilioni ya fedha tofauti na sasa. Si kila Rais atakayekuwa madarakani awe mkulima kama Nyerere la hasha!

Suala la ubia ni la maandalizi, Watanzania wazalendo wangeandaliwa kumiliki uchumi wao, wangekuwa tayari kutafuta watu wanaoweza kuwekeza nao kwa ubia.

Kumekuwepo na malalamiko ya viongozi wengi wenye hisa kwenye kampuni mbalimbali nje na ndani ya nchi na kubaki kuwa siri yao.

China iliachana na upuuzi huu na kwa yule anayebainika kufanya hivyo kwa siri, hukumu yake kupitishwa kwa kupigwa risasi hadharani ikiaminika ni msaliti.

Hoja ya ufisadi kuwakumba viongozi inapata nguvu kutokana na viongozi, familia zao na wanahisa wenzao kutofuata taratibu za manunuzi kiushindani. Uroho na ubinafsi ulitawala na hapa ndipo taifa lilipoanza kuyumba. Kama viongozi wangekuwa na dhamira njema, wangeshindwa kuiga mfumo wa China?

Tunayo mengi ya kujifunza kutoka China ya kuweza kugeuka kutoka kwenye uchumi wa dola na kuingia kwenye uchumi mkubwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari za SiasaTangulizi

Wabunge wacharuka kukatika kwa umeme

Spread the loveTATIZO la kukatika kwa umeme kila mara katika maeneo mbalimbali...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyookoa walemavu dhidi ya dhana potofu

Spread the loveMKOA wa Geita ni mmoja wa mikoa ya Kanda ya...

error: Content is protected !!