June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Serikali ihamasishe utalii wa ndani’

Twiga wakiwa Mbugani

Spread the love

SERIKALI imetakiwa kuwahamasisha Watanzania na kutoa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa utalii wa ndani. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Wito huo, umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya utalii ya Samesafaris, Amana Kazoka, alipokuwa akizungumza na MwanaHALISIOnline kuhusu umuhimu wa utalii wa ndani na uelewa wa nchini.

Kazoka amesema licha ya serikali kutambua umuhimu wa sekta ya utalii kwa kuliingizia taifa pato kubwa, bado Watanzania wazawa wametelekezwa.

“Inasikitisha kuona wageni wakitoka mbali kuja kuona wanyama, mito, maziwa, mlima Kilimanjaro, pango la Amboni na sehemu nyinginezo lakini Watanzania wengi hawana mwamko wa kutembelea hata mbuga moja ya wanyama.

“Kama serikali ingewahamasisha kwa kufanya utalii wa ndani, ni dhahiri kuwa serikali ingeingiza pato kubwa tofauti na ilivyo sasa na kuondoa kero mbalimbali kama vile ukosefu wa madawati katika shule, uboreshaji wa huduma za afya na uboreshaji wa miundombinu ambayo ipo chini ya halmashauri,”amesema.

Ameongeza kuwa, ili kupata kizazi chenye mwamko wa kudumisha wasuala ya utalii wa ndani ni vyema serikali ikapanga bajeti ambayo inaweza kutumika kuwasafirisha kwa awamu wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi sekondari kwa lengo la kutembelea maeneo mbalimbali iliwemo mbuga za wanyama.

“Wapo watoto ambao wamezaliwa mkoani Kilimanjaro lakini hawajawahi kufika mlima Kilimanjaro wala mbuga ya wanyama ya mkomazi na badala yake wanabakia kuona kwenye picha na wala hawana msukumo wa kutaka kutembelea maeneo hayo,”amesema.

Kazoka ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Samesafaris, amesema licha ya kupokea watalii kutoka nje ya nchi lakini amepania kuhakikisha anawahamasisha vijana wawe wanathamini na kutambua umuhimu wa utalii wa ndani.

Pia, amewataka Watanzania kujijengea tabia ya kutembelea maeneo mbalimali yaliyopo ndani ya Tanzania ili kujioneoa hali halisi ya taifa.

Sambamba na hayo ameitaka serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utaii kuziwezesha halmashauri ili ziweze kulinda, kutunza na kutangaza vivutio mbalimbali ambavyo vipo katika halmashauri husika.

error: Content is protected !!