August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali: Hakuna askari aliyetumwa kuua watu Loliondo

Spread the love

SERIKALI imesema hakuna kikosi cha askari waliokwenda kuua watu au kufukuza watu kutoka katika tarafa ya Loliondo na eneo la Kreta ya Ngorongoro mkoani Arusha kama ambavyo baadhi ya watu wanatangaza. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Pia imesema kwa bahati mbaya huko Loliondo watu wameshinikiza wananchi wafanye maandamano kuwafuata watu waliokuwa wanafanya zoezi la alama za uwekaji mipaka na kusababisha vurugu zilizochangia askari mmoja kupoteza maisha.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 12 Juni, 2022 jijini Dodoma na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akifafanua kuhusu zoezi hilo, Msigwa amesema Serikali inaendelea na kazi ya uwekaji wa alama ambazo zinapakanisha eneo ambalo wananchi wanatumia na eneo la hifadhi.

“Kilichotokea Loliondo ni kwamba serikali inaweka alama za mpaka kati ya eneo la hifadhi na eneo ambalo ndugu zetu wamasai wanalitumia, zoezi hili halijafanyika Loliondo peke yake limefanyika mengine kama Igombe.

“Bahati mbaya kule Loliondo watu wameenda kuwashinikiza wananchi wafanye maandamano kuwafuata watu wanafanya zoezi wakiwa mbali kutoka eneo ambalo wakazi wa Loliondo wanaishi.

“Wale wananchi waliokuwa wamehamasishwa wakaenda kuwavamia maofisa na watalaam na mafundi waliokuwa wakiweka zile alama wakamjeruhi askari mmoja na tumempoteza kwa sababu alichomwa mshale kichwani,” amesema Msigwa.

Amesema ni bahati mbaya sana hilo limetokea lakini serikali inasisitiza, kinachofanyika Loliondo hakuna askari aliyekwenda kumfukuza mwananchi Loliondo aondoke kwenye eneo lake.

Amesema eneo hilo lina kilomita za mraba 4000 ambapo Serikali kwa makubaliano na wananchi ilitenga, eneo la kilomita za mraba 2500 zitumiwe na wananchi na kilomita 1500 libaki kwa ajili ya hifadhi na ndivyo ilivyo.

“Watalaam hao walienda kuweka alama kwenye eneo hilo kuonesha kwamba hapa ni hifadhi na huku kubaki kwa wananchi, lakini watu wakahamasishwa wakajazwa maneno wakaenda kufanya hizo vurugu ambazo zimejitokeza.

“Tunawasihi sana wananchi wa Loliondo, tuheshimu taratibu, kama mna jambo viongozi wapo, milango ya serikali ipo, semeni maneno yenu yatasikilizwa na mtapatiwa majawabu lakini kwenda kuwaingilia maofisa ambao wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu na sheria si sawa.

“Jambo hili linafuatiliwa na wote wanaofanya uchochezi huu watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria, nawaomba sana waandishi wa habari tusishiriki uchochezi wa namna hii kwa sababu Lolindo hakuna uvamizi wa askari kwa wananchi,” amesema

Aidha, amesisitiza kuwa watu wasichanganye suala la Ngorongoro na Loliondo.

“Kule Ngorongoro kwenye Kreta… approach tuliyotumia ni hiihii, tumewaambia wananchi, kwamba hapa tunahitaji kupahifadhi, tunaendelea kuzungumza nao.

“Tumeandaa eneo kule Msomera Handeni Tanga, tunajenga nyumba, wale ambao wapo tayari kuondoka kupisha shughuli za uhifadhi wanaondoka na mpaka sasa tuna maombi ya kaya zaidi ya 293, zaidi ya wananchi 1400 wapo tayari kwenda kule kukaa.

“Kule akienda anapewa nyumba anapewa eneo la takribani heka tatu kwa ajili ya shughuli zake za kilimo, lakini pia tumetenga eneo kwa ajili ya ufugaji hayo ndio maisha ya kistaraabu ambayo tunataka,” amesema.

Amesema Serikali inataka watu sasa wawe wafugaji badala ya kuwa wachungaji, kwa hiyo dhamira ya serikali ni njema na jambo hilo linafanyika kwa mazungumzo.

“Hakuna mahali ambapo serikali imechukua silaha za moto kwenda kuwafuata wananchi kwa ajili kuwaambia wananchi tokeni. Hatukufanya hivyo,” amesema.

Amesema kilichotokea Loliondo, serikali inaendelea kulifanyia kazi na kulifuatilia wakati kule Ngorongoro inaendelea na mazungumnzo na wananchi wenye hiyari.

“Tumejenga nyumba 103 na nyumba nyingine 400 zinaendelea kujengwa tutaendelea kuwapa wananchi waliotayari kuhama watoke kule ili tukahifadhi lile eneo,” amesema.

Kuhusu taarifa za madiwani na baadhi ya wananchi wa tarafa hiyo ya Loliondo kutofahamika walipo tangu wakamatwe na askari polisi, Msigwa alisema hajapata taarifa hizo.

“Lakini wote waliohusika kuleta sintofahamu nchi ina sheria, sheria inachukua mkondo wake… uwe kiongozi usiwe kiongozi ni hatua za kisheria zinafuata mkondo wake.

“Tunaendelea kufuatilia kwa umakini, taharuki inayotengenezwa kwenye mitandao ya kijamii haina uhalisia,” amesema.

Pamoja na mambo mengine alisema Serikali imefuatilia hao watu wanaosema wameumia lakini katika hopsitali zote za Serikali hakuna majeruhi.

“Tunajaribu kuangalia nani anafanya hivyo, serikali ipo macho tunafuatilia, niwahakikishie watafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

error: Content is protected !!