October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali: Bomoabomoa kuendelea

Spread the love

SERIKALI mpya ya Dk. John Magufuli imesema itaendelea na uamuzi wake wa kubomoa makazi ya wananchi kwenye maeneo ya Bonde la Mto Msimbazi ambalo inayatambua kama “maeneo hatarishi.” Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hiyo ni kauli ya msimamo iliyotolewa na Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba mbele ya waandishi wa habari.

Waziri Makamba amesema uamuzi huo umefanywa baada ya kupatikana ripoti ya tathmini ya wataalam iliyoandaliwa na wizara mbalimbali ikiongozwa na wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Amewaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na tathmini ya kitaalam iliyofanyika, imebainika kuwa wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba zao zimebomolewa.

Kwa uhakiki uliofanyika, imebainika watu 20 tu ndio walikuwa na uhalali wa kuishi sehemu hizo na wakazi 199 walikuwa na vibali vya muda mfupi vya kuishi maeneo hayo.

Tathmini hiyo imefanywa na wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa (TAMISEMI) na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Maliasili na Utalii. Makamba amesema baada ya mkutano wa Mawaziri hao kwa niaba ya serikali uliadhimiria kuwa zoezi la kuwaondoa wananchi waishio katika Bonde la mto Msimbazi litaendelea kwa utaratibu ambao “hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi.”

Pia amesema kwamba zoezi la ubomoaji litajikita Bonde la Msimbazi tu ambako watakaohitajika kuhama ni wale ambao makazi yao yamo ndani kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya bonde, na kwenye kingo za mto. Lakini wakazi watakaokuwa na nyaraka zilizotolewa na mamlaka za serikali na zikiwaruhusu kuishi eneo hilo hawatahamishwa.

Katika hatua nyingine, waziri Makamba amesema ndani ya siku tatu zijazo, kutafanywa uzoaji au usawazishaji kifusi katika maeneo ambamo uvunjaji makazi ulifanywa.

Amesema kwamba serikali itaheshimu amri ya Mahakama kuhusu pingamizi iliyotolewa kwa baadhi ya wakazi wa mabondeni. Lakini pia serikali itafuatilia kwa ukaribu kesi iliyofunguliwa ili kesi hiyo “iishe na taratibu nyingine ziweze kuendelea.”

Amesema makubaliano yamefikiwa baada ya tathmini ya wataalamu kuwa upo umuhimu wa makazi yaliyoko kwenye maeneo hayo hatarishi kuondoshwa ili kuzuia matatizo yanayoweza kutokea kama vile mafuriko hasa zitakaponyesha mvua kubwa.

“Serikali haina dhamira ya makusudi kuwakomoa wananchi, lakini tunafanya hivyo kwa nia ya kuzuia maafa ya mafuriko,” amesema Waziri Makamba.

Amesema mwaka 2011 ziliponyesha mvua nyingi, kulitokea mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 49, kwa hivyo alisema serikali haipo tayari kuona matatizo yale yanatokea tena wakati ingeweza kuyakinga.

error: Content is protected !!