Spread the love

SENSA ya Watu na Makazi ya 2022, imepangwa kufanyika siku ya Jumatatu, tarehe 23 Agosti 2022. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Tarehe hiyo imetangazwa leo Ijumaa, tarehe 8 Aprili 2022, visiwani Zanzibar na Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua nembo na tarehe ya zoezi hilo.

“Napenda kutamka rasmi kuwa, tarehe 23 Agosti mwaka huu, ni tarehe ya sensa ya watu na makazi kwa hapa nchini kwetu Tanzania,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameomba viongozi wa dini na taasisi za kiraia, ziongeze nguvu katika jitihada za kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa zoezi hilo, ili kuondoa fikra potofu kuhusu uhesabiwaji watu.

“Tuna changamoto ya kimila, kuna watu wanaamini kuhesabishwa ni balaa na nuksi kuonesha una watoto wangapi. Kwa hiyo viongozi wa dini mtusaidie kuelimisha watu wetu. Kuna baadhi ya watu wanaficha watoto wenye ulemavu wasitolewe kuhesabiwa,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi, amesema Serikali inafanya sensa hiyo, kwa ajili ya kupata takwimu sahihi za idadi ya watu kwa ajili ya kupanga maendeleo.

“Nawaomba kila Mtanzania aliye hai ahesabiwe tujue idadi ili tukijipanga tujue tunajipanga kwa namna gani, mkawasomeshe wananchi kila mmoja aelewe tunahesabiwa ili kwenda sawa na hesabu zetu za maendeleo ya kiuchumi, hakuna sababu nyingine iliyofichwa,” amesema Rais Samia.

Akizungumzia nembo ya sensa, Rais Samia ameagiza itumike katika shughuli za Serikali na sekta binafsi, kwa ajili ya kuitangaza kwa wananchi.

“Wito wangu nembo hii itumike kuanzia itakapozinduliwa kwa shughuli ya sensa hadi itakapokamilika shughuli za sensa. Shughuli zote za Serikali na sekta binafsi tumieni nembo hii kuitangaza sensa kwa kuiweka katika tovuti zenu na taasisi zitakazokuwa na vipindi katika Tv zenu nembohizi zitumike,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Sekta binafsi nembo zinazoweza kuwekwa kwenye bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ikiwemo kwenye maji, risiti. Kila kinachotumika basi nembo ya sensa ionekane.”

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amewahimiza wataalamu na viongozi wa Serikali na sekta binafsi, kuongeza kasi katika matumizi ya takwimu kwenye kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.

“Serikali zetu zinajitahidi kujua idadi ya watu katika kila familia na maeneo ya utawala ili kuimarisha utoaji huduma za jamii na ujenzi wa miundombinu, aidha utekelezaji uchumi kwa njia za kidigitali inahitaji kujua taarifa zao, utoaji taarifa sahihi utasaidia kutekeleza mipango yetu,” amesema Rais Mwinyi.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Taufa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, amesema maandalizi ya zoezi hilo yamefikia asilimia 79.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *