May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sengerema yazidiwa wagonjwa Korona, mbunge aiangukia Serikali

Spread the love

 

MBUNGE wa Sengerema mkoani Mwanza (CCM), Hamis Tabasam, ameiomba Serikali iipatie msaada wa dharura wa vifaa tiba vya kutibu Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19),  Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, ili kunusuru maisha ya wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza…(endelea).

Tabasam ametoa ombi hilo leo Jumatatu, tarehe 9 Agosti 2021, alipoitembelea hospitali hiyo kwa ajili ya kuangalia utendaji wake, katika kuwatibu wagonjwa wa Korona.

Tabasam amesema kuwa, hospitali hiyo imeelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa, ambao wanahitaji msaada wa kupumua kwa kutumia mashine ya oksijeni.

Mbunge huyo amesema, hospitali hiyo inakabiliwa na ukata wa mitungi ya oksijeni, ambao uwezo wake kwa siku ni mitungi 10, idadi isiyo kidhi mahitaji ya wagonjwa.

“Hospitali imeelemewa na wagonjwa, katika kuelemewa kwake ni kwamba, gharama za matibabu kusaidia wagonjwa waweze kupona ni kubwa, mgonjwa anahitaji mtungi mmoja mpaka mitatu kwa siku, uwezo wa hospitali ni  mitungi10,” amesema Tabasam.

Kufuatia ukata huo, Tabasam ameiomba Serikali itoe msaada wa mitungi ya gesi ya oksijeni,  pamoja na vifaa tiba vingine katika hospitali hiyo.

“Tunamuomba waziri wa afya (Dk. Dorothy Gwajima), waziri mkuu (Kassim Majaliwa), katika kitengo cha majanga, Sengerema aione kwa jicho la huruma,  hali ni mbaya katika hospitali. Watueletee mitungi kwa haraka, la siyo itakuwa janga kubwa,” amesema Tabasam.

Aidha, Tabasam ameipa hospitali hiyo msaada wa Sh. 3.5 milioni, kwa ajili ya kujaza mitungi 100 ya gesi ya oksijeni.

“Watanzania wanaoguswa na hospitali za kiroho zinazofanya huduma watoe michango yao Mungu atawalipa,  mtungi mmoja gharama inafika Sh. 200,000 mpaka 300,000 , gharama za kununua mitungi zaidi ya 200 hatuna,” amesema Tabasam na kuongeza:

“Mimi kama Tabasam nachangia ujazaji mitungi 100, sawa na Sh. 3.5 milioni,   mifuko miwili ya sabuni za kunawia na barakoa 1,000.”

error: Content is protected !!