November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Selasini akoleza moto uenyekiti Chadema

Spread the love

MBUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Rombo, mkoani Kilimanjaro, Joseph Selasini, ameonya kuwa hatua yeyote ya kuminya demokrasia ndani ya chama chake, yaweza kukigharimu chama hicho. Anaripoti Yusuph Katimba … (endelea).

Katika andishi lake alilolisambaza kupitia mitandao ya kijamii, Selasini amesema, “matusi” yanayoelekezwa dhidi ya mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe, “hayawezi kuvumilika.”

Mwambe alinukuliwa na vyombo vya habari, Jumamosi iliyopita akisema, muda ukifika, amedhamiria kujitosa katika kinyang’anyiro cha uenyekiti ndani ya Chadema.

Anasema, anamshukuru sana mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe, kwa mchango wake alioutoa katika chama. Anasema, kwa maoni yake, muda wa kiongozi huyo kuwaachia wengine kazi hiyo, umefika na kwamba amejipima na kujiridhisha kuwa anaweza kuifanya kazi hiyo kwa ukamilifu.

Hata hivyo, mara baada ya kutangaza mkakati wake huo, baadhi ya wapinzani wake wamekuwa wakimshutumu kuwa uamuzi wake huo umetokana na kutuhumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwambe alijunga na Chadema mwaka 2015 na kwamba baadhi ya wanaompinga wanauchukua ugeni wake kwenye chama kama mkakati wao wa kumpinga.

Lakini Selasini akizungumzia madai hayo anasema, “hiki ni chama cha kidemokrasia. Na hivyo ni sharti kitende mambo yake kwa kufuata misingi hiyo. Tunaposhindwa kusimamia demokrasia ndani ya chama chetu, tunapata wapi msuli wa kudai kuwa ndani ya nchi hakuna demokarsia?”

Anaongeza, “mheshimiwa Mwambe, ni kiongozi wa chama. Ni mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kusini na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC). Tunapomshambulia kwa matusi na kejeli, tunatoa picha gani kwa walio nje ya mfumo wa Chadema?”

Selasini ametoa kauli hiyo siku mbili baada ya Mwambe kunukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema, anakusudia kuwania uenyekiti wa taifa wa chama chake.

Akizungumzia mwenyekiti wa sasa, Selasini amesema, “ni kweli kuwa mheshimiwa Mbowe amefanya mambo mengi sana. Na ni ukweli usioweza kujificha au kufichwa, kwamba chama hiki kuna mchango wake mkubwa.”

Hata hivyo, Selasini anahoji, “ …lakini ni wapi kwenye katiba yetu, panapoonyeshwa uchaguzi usifanyike au kiongozi aliyefanya mengi mazuri na mvumilivu apite bila kupingwa?”

Selasini ambaye pia ni Kaimu mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, mwenyekiti wa mkoa wa Kilimanjaro na  Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema, hawawezi kumtuhumu Rais John Magufuli kusigina katiba na sheria za nchi, wakati nao wanafanya hivyo hivyo.

“Kwani katiba yetu si inamruhusi kila mwanachama kugombea nafasi yoyote ndani ya Chama? Kama hivyo ndivyo, kosa la Mwambe liko wapi? Kama nakosea, naomba nisahihishwe,” ameeleza Selasini.

Anasema, “leo tuko na Mbowe na tunafikiri hakuna mwingine. Je, hatuungi mkono hoja zote za CCM dhidi ya Mbowe? Nilidhani akipata wagombea wenzake hata wanne na akapita, ataimarika zaidi na chama kitaonekana kuwa cha kidemokrasia na kuuwa kabisa hoja za kina Kibajaji Lusinde na Msukuma.”

Kuhusu suala la Mwambe kushika Ilani ya uchaguzi ya CCM, Selasini anahoji, “mbona kile ni kitabu tu? Mbona Waislam wanashika biblia ya Wakristu? Hata shati la kijani mbona wengi waliokuwa CCM wanayo? Mhe Bulaya, Mhe Sumaye na wengine hawana?”

Akiandika kwa ukali, Selasini anasema, “naomba matusi haya pelekeni au elekezeni CCM sio wenyewe kwa wenyewe na nadhani hata wanachama wengine waje tu chama kitachangiwa pesa za kutosha kupitia fomu za kugombea nadhani ni milioni 5 siyo haba.”

Tangu Mwambe atangaze kuwania wazifa huo wa juu kabisa ndani ya Chadema, kumeibuka matusi, kejeli na tuhuma lukuki dhidi yake, yeye mwenyewe akisema, “Niguse, Ninuke.”

error: Content is protected !!