KAMA ilivyokuwa katika kesi za watu maarufu zilizosababisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kufurika watu, hivi ndivyo ilivyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jana, anaandika Faki Sosi.
Watu wengi walijitokeza kwenye mahakama hiyo kumshuhudia Salum Njewete (34), mwalimu wa sanaa za mapigano (karate) maarufu Scorpion.
Scorpion alipandishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa madai ya wizi wa kutumia silaha na kuwatoboa macho watu.
Mbele ya Adolf Sanchore, Hakimu wa mahakama hiyo, Munde Kalombola ambaye ni mwendesha mashtaka wa serikali amedai kuwa, tarehe 6 Septemba mwaka huu katika maeneo ya Buguruni Shell, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alimvamia na kumchoma visu machoni, tumboni na mabegani Said Mrisho.
Kalombola amedai, mshtakiwa alimpora mkufu wa fedha gramu 38 wenye thamani ya Sh. 60,000, kidani cha mkononi chenye thamani ya Sh. 85,000 na fedha taslimu Sh. 331,000.
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 19 Oktoba mwaka huu.
Hali ilivyokuwa mahakamani
Mtuhumiwa alifikishwa mahakamani hapo jana akiwa amevaa fulana nyekundu na suruali aina ya ‘Jeans,’ alishuka katika karadinga la Magereza chini ya ulinzi mkali huku akificha sura yake kuogopa kamera za waandishi wa habari.
Umati mkubwa wa watu ulifurika katika viwanja vya mahakama ya Ilala kumshuhudia mshtakiwa ambaye jina lake limetikisa kwa sasa jijini Dar es Salaam kutokana na kutoboa macho.
More Stories
Dk. Mpango azitaka mamlaka maliasili utalii kukomesha urasimu vibali
TANESCO yaghairi matengenezo mfumo wa LUKU
Morogoro yapokea bilioni 111 miradi ya maendeleo