
Marehemu Edson Kamukara enzi za uhai wake
MISA ya shukrani ya kumbukumbu ya Marehemu Edson Kamukara itafanyika Jumamosi 15 Agosti, 2015 saa 8.00 mchana katika kanisa la Parokia ya Mt. Mashahidi wa Uganda lililopo Magomeni, jijini Dar es Salaam. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Marehemu Kamukara wakati wa uhai wake, alikuwa mhariri mwajiliwa wa gazeti hili la MwanaHALISI Online, linalomilikiwa kampuni ya Hali Halisi Publisher Limited. Alifariki 25 Juni mwaka huu nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam na kuzikwa 27 Juni kijijini kwao Ihangiro, Muleba Kusini mkoani Kagera.
Ibada hiyo imeandaliwa na Jumuiya ya wanafunzi waliosoma Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Kampasi ya Mwanza, wanaoishi jijini Dar es salaam.
Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mwenyekiti wa jumuia hiyo, Deogratius Temba, amesema “Ibada hiyo itawaleta pamoja marafiki wa karibu na rafiki yetu mpendwa marehemu Kamukara. Tunapenda kuwatangazia marafiki zetu wote, wanahabari, wanahariri, ndugu zake na waalimu wake kushiriki tukio hilo muhimu.”
“Kwa kuwa tunatambua mchango mkubwa wa Marehemu Kamukara katika ujenzi wa taifa letu kupitia taaluma yake ya habari, tunawaomba watu wote washiriki ibada hii ili kuendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha sisi na kusheherekea maisha ya Edson hapa duniani hasa mapambano dhidi ya ukuaji wa demokrasia nchini,” amesema Temba.
Temba amesema Katika ibada hiyo, wao kama marafiki zake wataweka bayana mkakati wao wa kuendelea kumuenzi Marehemu Kamukara na kuutambua mchango wake wakati wa uhai wake.
More Stories
Kifo cha mtawa: Ni simulizi nzito
TAKUKURU: Rushwa ya ngono ipo, fichueni
Usiyoyajua kuhusu Panya wapima TB