May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sare ya Azam FC, Simba wamkingia kifua kocha

Spread the love

 

BAADA ya kutoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Azam FC, klabu ya Simba kupitia msemaji wake, Haji Manara imesema, mashabiki wa klabu hiyo hawapaswi kumlaumu kocha wala mchezaji, kwani wapinzani wao ni bora na wana wachezaji wazuri. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mchezo huo wa kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulichezwa jana majira ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam na timu zote mbili kugawana pointi moja moja.

Manara amesema hayo kupitia video fupi iliyowekwa kwenye ukurasa wa Simba unaopatikana kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram na kueleza kuwa, licha ya Simba kuwa na timu bora lakini kuna muda unaweza usipate matokeo mazuri uwanjani japokuwa kusudi lako ni kushinda.

“Kuna wakati utakusudia kushinda lakini haiwi hivyo kuna wakati utafungwa au kutoka sare.

“Kuna siku timu bora yenye kila aina ya mchezaji na kila kitu, lakini inaenda kufungwa na timu ya kawaida na sijawahi kusema Simba tutashinda kila mechi,” alisema Manara.

Msemaji huyo aliendelea kwa kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kuwapongeza wachezaji katika mchezo wa jana kwani matumaini ya ubingwa bado yapo.

“Nawaomba mashabiki wetu tuwapongeze wachezaji maana tungeweza kufungwa, ila naomba niwaweke sawa kila kitu kipo vizuri na nafasi ya ubingwa bado ipo kama ilivyokuwa hapo awali,” aliongezea Manara.

Kuibuka huko kwa msemaji huyo kumekuja kutokana na maneno mengi ya mashabiki wa klabu hiyo mara baada ya kutoka sare kwenye mchezo ambayo timu yao ilicheza vizuri kipindi cha kwanza kwa kutengeneza nafasi nyingi za mabao lakini walishindwa kuzitumia.

Aidha hisia kali zinakuja kutokana na ushindani uliopo sasa kwenye ligi dhidi ya watani zao Yanga ambao wapo kileleni kwenye msimamo na kama Simba angeshinda mechi zake zote wangewafikia kwa pointi na kuongoza ligi hiyo kwa tofauti za mabao.

Kwa matokeo hayo ya jana Simba inaendelea kusalia kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 39, baada ya kucheza michezo 17, huku watani zao Yanga wakiendelea kusalia kileleni wakiwa na pointi 44 mara baada ya kucheza michezo 18.

error: Content is protected !!