MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mzee Phillip Mangula, amewaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho, kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Mzee Mangula ametoa wito huo leo Ijumaa tarehe 30 Aprili 2021, jijini Dodoma, saa kadhaa kabla ya wajumbe hao kufanya uchaguzi huo.
Mkutano huo maalum wa CCM umeitishwa kwa ajili ya kujaza nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho, iliyoachwa wazi na Hayati Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, ambapo Rais Samia, alipitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mzee Mangula aliwaomba wajumbe hao kumchagua Rais Samia kuwa mwenyekiti wa CCM, akisema kwamba ana uwezo wa kukiongoza chama hicho, kwa kuwa ana uzoefu kutoka kwa Dk. Magufuli.
Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa Ccm
Amesema, Rais Samia alizunguka katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na 2020, kuinadi Ilani ya chama hicho, ambapo yeye alikuwa mgombea mwenza huku Dk. Magufuli akiwa mgombea wa Urais wa Tanzania.
“Wakati wa kuomba uongozi 2015 ndiyo awamu ya tano imeingia madarakani, kulikuwa mgombea na mgombea mwenza na walizunguka nchi nzima kutangaza mambo ambayo CCM kingeyafanya katika miaka mitano hiyo (2015-2020),” amesema Mzee Mangula.
Mwanasiasa huyo mkongwe Tanzania amesema “wawili hawa walikuwa ni Dk. Magufuli kama mgombea na mgombea mwenza akiwa Samia, katika kipindi cha miaka miaka mitano walifanya kazi nzui sana , kwa uthibitisho, ilipoingia 2020 wawili hawa waliungwa mkono na wapiga kura kwa asilimia zipatazo 85.”
Amesema, kutokana na uongozi mzuri wa Dk. Magufuli na Samia, Watanzania waliwachagua tena kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Maana yake ni kwamba wananchi waliikubali kazi yao wanayoifanya wawili hao, pia wabunge katika majimbo yao walitangaza nini chama kingefanya awamu ya tano, ndio maana wabunge katika majimbo yao walishinda na kuwa wabunge kwa kutangaza ahadi ya CCM ni zaidi ya asilimia 90 ya majimbo yote,” amesema Mzee Mangula.
Leave a comment