WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamemchagua kwa asilimia 100, Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa Mwenyekiti wa chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Ni rekodi nyingine kwa Samia, kuwa mwenyekiti wa kwanza mwanamke na Rais wa kwanza mwanamke nchin Tanzania.
Rais Samia, amechaguliwa leo Ijumaa, tarehe 30 Aprili 2021, katika mkutano huo, uliofanyikia ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Akitangaza matokeo hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema, wajumbe wa mkutano huo walikuwa 1862 na ndio waliopiga kura.
Amesema, hakuna kura ya hapana na kura za ndio ni 1862 sawa na asilimia 100.
Rais Samia, amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Hayati Rais John Pombe Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.
Mwili wa Hayati Magufuli, ulizikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.
Kutokana na kifo hicho, Samia aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania na kuandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania.
Pia, leo Ijumaa, Rais Samia ameandika historia nyingine ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbali na rekodi hiyo, Samia aliweka nyingine ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa Rais wa Tanzania.
Leave a comment