RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuahidi Rais mpya wa Tano wa Kenya, Dk. William Ruto kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu katika kuleta maendeleo ya pamoja ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi hizo na ukanda wote wa Afrika Mashariki. Anaripoti Mwandishi wetu … (endelea)
Pia amewapongeza Wakenya kwa kuonesha uikomavu wa demokrasia na kumaliza uchaguzi mkuu wa taifa hilo salama na sasa tupo wakenya na Afrika Mashariki wanashangilia uapisho wa rais huyo mpya.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo wakati akihutubia katika sherehe za uapisho wa Rais mteule Dk. William Ruto kuwa Rais wa Tano wa Kenya.
Sherehe hiyo imefanyika katika uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani Nairobi.
Rais Samia mbali na kumpongeza Ruto pamoja na Naibu wake Rigathi Gachagua kwa kupokea rasmi jukumu la kuiongozi Kenya, pia amemshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kumaliza vema kuitumukia nchi yake na kwa mafanikio makubwa.
“Tunawapongeza kwa kuonesha uikomavu wa demokrasia na kumaliza uchaguzi salama na leo tupo hapa pamoja kama wakenya na Afrika Mashariki tunashangilia uapisho wa rais wetu mpya.
“Nataka niwaambie kama kuna zawadi mlioitoa kwa Afrika Mashariki mwaka huu ni zawadi ya amani mliyoiweka katika uchaguzi. Tunawashukuru sana, kwa zawadi hiyo muhimu.
Amesema kwa kuwa uchaguzi umemaliza sasa wananchi wote wa Kenya washikane mikono kuijenga Kenya.
“Mwisho kama dada nitumie fursa hii kuihakikisha Kenya dhamira yetu ya dhati ya kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuleta maendeleo ya pamoja ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zetu na ukanda wote wa Afrika Mashariki.
“Namuomba Mwenyezi Mungu amuwezeshe ndugu yetu Ruto pamoja na serikali atakayoiunda awatie nguvu ili waweze kutumikia vema nchi hii katika kiwango kinachotarajiwa na wananchi wa Kenya. Mwenyezi Mungu aibariki Kenya na Afrika Mashariki,” amemaliza Rais Samia.
Leave a comment