August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Samia ampa onyo RC Chalamila: Nategemea umekua sasa

Albert Chalamila

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amempa onyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila, ambaye amerejesha uongozini baada ya kumwondoa Juni 2021 akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza mara baada ya uapisho leo Jumatatu tarehe Mosi Agosti, 2022, mkuu huyo wa nchi amemtaka Chalamila kutuliza kichwa na kwenda kumsaidia kazi katika eneo alilopangiwa.

“Mwanangu Chalamila mategemeo yangu umekua sasa akili imetulia, wewe ni mfanyakazi mzuri lakini mtundu mno sasa nlikuacha nje kipindi hicho nimeamua kukurudisha sasa ukakue utulize kichwa ukanisaidie kazi eneo ulilopangiwa,” amesema Rais Samia.

Aidha alimwonya kuwa kuteuliwa kwake haimaanishi kuwa amemalizana naye, “ninakuangalia kwa karibu sana.”

Utenguzi wa Chalamila ilihusishwa na kauli yake ya kuwaambia wananchi wa Mwanza kufika na mabango katika tukio ambalo Rais alikuwa mgeni rasmi na kuandika chochote wanachotaka.
Hilo limedhihirika leo baada ya Rais mwenyewe kuita jina la Chalamila katika hafla hiyo na kukumbushia kauli yake ya kutaka wananchi kuja na mabango.

“Chalamila upo eeh, wale wanaoandika mabango sasa mkawaambieni andikeni tu chochote njooni nayo,”

“Yakija mabango maanake wananchi wanalalamika na kama wanalalamika wewe uliopo hapo maanake hufanyika kazi yako vizuri, wananchi wanakuja na mabango mapema mnayachukua mnayaficha, mnawanyima haki yao maana hayo ndo mdomo wao wa kusemea.

Alifafanua, “mimi nilisema sitaki kuona mabango kwasababu nilitaka mwende mkafanye kazi zenu, kama nikiona mabango maana yake hamfanyi kazi.”

error: Content is protected !!