October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Samia akemea wazazi wanaowapa watoto ulanzi

Spread the love

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wazazi na walezi wa mkoa wa Iringa kuacha kuwapa watoto wao pombe ya kienyeji aina ya ulanzi badala yake wahakikishe watoto hao wamepata milo mitano kwa siku. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 13 Agosti, 2022 wakati akihitimisha ziara yake katika mkoa wa Iringa kabla ya kuelekea Dodoma.

Amesema kumekuwa na hulka ya wazazi kuwapa watoto wao ulanzi kidogo ili walale muda mrefu kisha wao kuelekea shambani kulima.

“Ule muda unaomlaza mtoto anakosa milo miwili katikati ilihali mtoto anatakiwa awe na milo mitano kwa siku. Lakini hapa unampa uji asubuhi na ka-ulanzi kidogo unamlaza unakwenda shamba… unarudi saa nane.

“Hapo katikati amekosa milo miwili au  kama ulimuachia uji dada yake kwamba mdogo wake akiamka ampe uji, naye anakunywa huohuo uji hivyo mtoto anapata kidogo,’ amesema.

Awali Waziri wa Afya, Waziri Ummy Mwalimu amesema katika mkoa wa Iringa kuna tatizo kubwa la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Amesema kiwango cha udumavu mkoani humo ni asilimia 47 ambapo katika kila watoto 100, watoto 47 wamedumaa.

“Tunazungumzia kuboresha elimu, afya, miundombinu  na vingine vingi lakini kama watoto wamedumaa hawawezi kufundishika hatutakuwa madaktari, walimu wahandisi wazuri.

“Tunapovua samaki tusiuze wote tuwape watoto wetu, tunywe maziwa tutapunguza watoto wanaoumwa hovyo,” amesema.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Salim Asas amesema shamba la Asasi ni miongoni mwa mashamba yanayozalisha maziwa kwa wingi lakini kwa masikitiko makubwa watu mkoa huo watoto wao wamelemaa.

“Ndugu wanyalukolo tuache kuwapa watoto ulanzi! Mpaka tumetengeneza maziwa yanaitwa kiduchu kwa ajili ya watoto lakini hamnunui… mnanunua ulanzi. Tunaomba mjitahidi kuwapa watoto wetu lishe bora,” amesema.

error: Content is protected !!