SERIKALI ya Tanzania, imeagiza wizara, taasisi za umma na binafsi kutumia maonesho ya kilimo ‘Nanenane’ kama jukwaa la wakutanisha wadau wake, kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Simiyu … (endelea).
Agizo hilo limetolewa leo Jumamosi tarehe 1 Agosti 2020 na Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wakati anafungua maonesho ya Nanenane mkoani Simiyu na yatahitimishwa tarehe 8 Agosti 2020.
Mama Samia amezitaka wizara pamoja na taasisi hizo, kuwekea mkazo wa changamoto za ukosefu wa masoko, mifumo ya upatikanaji mitaji, maeneo ya uwekezaji pamoja na miundombinu ya usafirishaji, uchukuzi na uhifadhi.

“Kila wizara, taasisi za umma na binafsi ziwe mstari wa mbele kuwakutanisha wadau wa sekta husika, kujadili changamoto zilizopo,”amesema.
“Suala la masoko, miundombinu ya usafirishaji, uchukuzi na na uhifadhi iwe kipaumbele katika majadiliano yenu, suala hili lifanye katika maonesha kote nchi,” amesema Mama Samia.
Mama Samia amesema, Serikali ya awamu ya tano imefanya kazi kubwa katika kuongeza mnyororo wa uzalishaji na thamani ya bidhaa za kilimo kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
“Nyote ni mashahidi wa kazi zilizofanywa na awamu ya tano ikiwa ni pamoja na kusimama na wakulima katika mnyororo mzima wa uzalishaji na uongezaji thamani bidhaa za kilimo. Kupitia Ilani ya CCM mwaka 2015/20 tumetekeleza ahadi tulizotoa kwa wakulima,” amesema Mama Samia.
Leave a comment