October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Samia aagiza maofisa uhamiaji waliohusika ubadhirifu viza kushughulikiwa

Spread the love

 

RAIS wa Jamhurii ya uungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Kamishna Jenerali wa Jeshi La Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, “kuwashughulikia” maofisa wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za viza na vibali vya wageni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga … (endelea).

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Jumatatu tarehe 15 Agosti, 2022, wakati akifunga mafunzo ya awali ya askari wa uhamiaji kozi namba 1 ya mwaka 2022, katika chuo cha uhamiaji Kichakamwiba mkoani Tanga.

“Nimesikia baadhi ya maafisa uhamiaji ambao sio waaminifu na hii kuna kesi kwenye mafaili sasa hivi, fedha zinazotolewa za visa, fedha zinazotoka za vibali wanazigeuza za kwao na wanaziweka mifukoni,” amesema.

Ameongeza kuwa katika utafiti mdogo uliofanywa mapema mwaka huu, askari wa uhamiaji “hasa” kwenye vituo vya Zanzibar na Dar es Salaam wamegundua upotevu “mkubwa” wa fedha za visa ambao unafanywa na maafisa wa uhamiaji.

“Vitendo vya aina hii viende vikakomeshwe ndani ya jeshi hili na turudi kwenye maadili ya jeshi,” amesema Rais Samia.

Kutokana na tuhuma hizo Rais Samia amemuagiza Kamishna wa Uhamiaji kuhakikisha wale wote waliohusika na vitendo hivyo wanashughulikiwa.

“Washughulikiwe ili kutoa taswira kwamba anayekosea ndani ya jeshi anashughulikiwa na wengine wapya, watoto hawa hawatakiwi kuiga vitendo vya kaka na dada zao wanaowakuta,” amesema Rais Samia na kuongeza;

“Mkiwashughulikia wale hawa watajua vitendo vya kuchukuliana nidhamu vipo na adhabu zipo. Kwahiyo naomba sana Kamishna simamia hilo.”

Amesema Serikali itashindwa kuvumilia endapo Kamishna Jenerali huyo atashindwa kuchukua hatua kwa yale ambayo Serikali inayabaini na kumwonesha.

“Niwatake wote kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kutoa huduma bora zaidi kwa wageni na wananchi kwa ujumla, watakao kwenda kinyume na hivyo Kamishna unajua chakufanya lakini sisi kama serikali hatutayavumilia, tutakapoyasikia tutakuletea tutaangalia ni hatua gani unachukua lakini tukiona mambo hayaendi tutashindwa kuvumilia,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa huko katika vituo imeshuhudiwa vitendo vya rushwa vinavyofanywa na maofisa wa uhamiaji sambamba na unyanyasaji wa wageni wanaoingia nchini.

Kutokanana hali hiyo Rais Samia ameshauri askari wote waliopo vituoni warudi vyuoni Kwenda kujifunza na wale waliohitimu Kwenda kuchukua nafasi hizo.

error: Content is protected !!