August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mgomo wa Maalim Seif kwa Dk. Shein watikisa CCM

Spread the love

KITENDO cha Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kukataa kumsalimia kwa kumpa mkono, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kinaendelea kukiumiza Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Charles William.

Maalim Seif, alizua gumzo mwanzoni mwa wiki hii baada ya kuinamisha kichwa chini kana kwamba haoni uwepo wala hasikii sauti ya Rais Shein, aliyekuwa akimsalimia kwa maneno na kumpa mkono pasipo mafanikio. Wawili hao walikutana katika msiba wa Aboud Jumbe, Rais Mstaafu wa Zanzibar.

Kitendo hicho, kinatajwa kama kielelezo cha chuki na uhasama mkubwa wa kisiasa baina ya wawili hao pamoja na vyama vyao huku wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wakionya kuwa, uhasama huo ukiendelea, unaweza kuleta athari kubwa.

Vuai Ali Vuai, Naibu Katibu Mkuu CCM- Zanzibar, katika hali inayoashiria kuchukizwa na kitendo cha Maalim Seif amesema, sasa ni wakati muafaka kwa serikali ya Zanzibar kumtenga na kumzuia mwanasiasa huyo kuhudhuria katika hafla za kitaifa.

“CCM tumehuzunishwa na tumefedheheshwa sana na kitendo cha Maalim Seif ambaye pia aliwahi kuwa kiongozi wa ngazi za juu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miaka ya nyuma. Kiukweli hatukutarajia kabisa angefanya kitendo kama kile.

Ni vyema sasa akazuiliwa kushiriki katika hafla za kitaifa ambazo viongozi wa hadhi yake hupewa nafasi na heshima ikiwemo kukaa mbele na viongozi wengine wa kitaifa. Amefanya vile kwenye msiba, je akialikwa katika hafla ya kitaifa si atafanya zaidi ya vile?” amesema Vuai.

Tangu Maalim Seif kukataa salamu ya Dk. Shein katika shughuli ya msiba wa Jumbe, rais wa awamu ya pili wa Zanzibar kumekuwa na maoni tofauti ya watu juu ya kitendo hicho huku katika mitandao ya kijamii kukiwa na kampeni maalum ya kupiga picha za kuunga mkono kitendo hicho.

Watu wamekuwa wakipiga picha wakiwa wawili, mmoja akionekana kumsalimia kwa kumpa mkono mwenzake na anayepewa mkono akionekana kukataa kupokea mkono na kuinamisha kichwa chini.

Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu CUF-Zanzibar amenukuliwa akisema, “Kutokana na dhuluma hizi tulizofanyiwa na serikali ya Dk. Shein, rais huyo anastahili kupewa mkono? Hapana, hapana. Tunafanya hivi ili kupinga hoja kwa amani.”

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!