August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakaya: Kilimo, Mifugo kwanuka ufisadi

Spread the love

WATENDAJI katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wameelezwa kuingia mikataba ya ovyo kwenye baadhi ya Vyama vya Ushirika ikiwa ni pamoja na usimamizi mbovu, anaandika Regina Mkonde.

Magdalena Sakaya, Waziri Kivuli katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amesema hay oleo wakati akitoa hotuba kuhusu mapitio ya utekelezaji wa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa 2016/2017 mjini Dodoma.

Wakati akisoma hotuba hiyo, Sakaya amesema kuwa, Vyama vya Ushirika vya kilimo nchini viko katika hali mbaya kiuchumi kwa kuwa, Maofisa Ushirika wenye jukumu la kufanya ukaguzi kisheria kwenye vyama vya ushirika, wameshindwa kutimiza wajibu huo huku baadhi yao wakishirikiana na viongozi wa ushirika kuhujumu vyama hivyo.

“Kutokana na ubadhirifu mkubwa uliojitokeza kwenye vyama vya ushirika vya Mkoa wa Tabora kuanzia chama kikuu WETCO, Serikali kupitia aliyekuwa waziri mwenye dhamana ya kilimo Prof. Jumanne Maghembe iliagiza kufanyika ukaguzi maalum Mkoa wa Tabora na taarifa ikapatikana,” amesema na kuongeza;

“Kambi rasmi ya upinzani inauliza je, ni kwa nini hadi leo wahusika wa ubadhirifu huo hawakuchukuliwa hatua? Serikali inaliambia nini bunge hili?

“Agizo la waziri kuwa wahusika wafikishwe mbele ya sheria mbona halijatekelezwa hadi sasa?”

Kwa upande wa kunufaisha wakulima wa zao la tumbaku ameeleza kuwa, mwaka wa fedha wa 2014/2015 wakati waziri aliyekuwa na dhamana ya kilimo alipokuwa akiwasilisha bajeti yake.

Amesema kuwa, serikali ilitafuta wanunuzi wa tumbaku kutoka Korea na China ili kuongeza ushindani kwa kampuni zinayonunua tumbaku kutoka kwa wakulima jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.

“Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua utekelezaji wa mpango huu umefika wapi? Wanunuzi hao wameshafika au bado wako njiani?

Sakaya ameeleza kuwa, mashamba mengi ambayo yalikuwa yanamilikiwa na serikali yaliyokuwa yanazalisha vizuri ambayo serikali iliamua kuingia ubia au kuyauza.

Mikataba mingi ya ubia iliingiwa bila kuzingatia masilahi ya Taifa na badala yake ilizingatia zaidi masilahi binafsihuku akitaja mifano ya mikataba hiyo ikiwemo mikataba ya ubia ya Kampuni ya Kilombero Plantations Ltd (KPL) na Mgololo.

“Mkataba ulioingiwa na serikali kupitia RUBADA na kampuni ya KPL ambapo kabla ya mkataba huo RUBADA ilikuwa na mbia mwingine wa Kikorea akiitwa Kotako ambaye alikuwa na majengo, mashine za uzalishaji, matrekta, magari, na mashmba ya mngeta,” amesema na kuongeza;

“Lakini kwa sasa baada ya Kotako kuondoka maana yake RUBADA ndiye mmliki wa hisa asilimia 5 na KPL wanamiliki hisa 95 ambao hawakuwekeza zaidi ya kukuta kila kitu site na kuanza kuuza na kukodisha mashine na mashamba kwa wakulima.”

Sakaya amesema kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa sasa ni muda muafaka wa kuiangalia na kuipitia upya mikataba yote iliyokuwa imeingiwa na serikali na wawekezaji na kuona kama kweli ina masilahi kwa nchi au iliangalia zaidi masilahi binafsi kutokana na kugubikwa na ufisadi.

error: Content is protected !!