Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sakata la Tril. 1.5 majibu ni haya
Habari za SiasaTangulizi

Sakata la Tril. 1.5 majibu ni haya

Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Spread the love

BUNGE limetoa ufafanuzi kuhusu ‘upotevu’ wa kisasi cha Sh. 1.5 trilioni zilizoelezwa kutojulikana matumizi yake katika Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2016/17. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Chombo hicho cha kutunga sheria kimeeleza kuwa, kilichosababisha mkanganyiko huo ni taarifa ya awali iliyopelekwa na Hazina kwamba makusanyo yalikuwa Sh. trilioni 25.3 na baadaye kupeleka taarifa mpya kwamba Makusanyo ya Mfuko Mkuu wa Serikali yalikuwa Sh. 23.8 trilioni.

Akizungumzia matokeo ya uchambuzi wa ripoti ya CAG 2016/17 bungeni jijini Dodoma tarehe 1 Februari 2019, Naghenjwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) amesema, kilichotokea kimesababishwa na kuwepo taarifa mbili za viwango na kwamba, kiwango cha pili kilichotolewa na Hazina (Sh. 23.8 trilioni) ndicho kilichokusudiwa.

Kauli ya Kaboyoka inatokana na mjadala ulioibuliwa na Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo mwaka jana Aprili wakati wa Bunge la Bajeti alipohoji zilipo fedha hizo.

Kaboyoka ameliambia Bunge kuwa, Hazina ilipeleka taarifa mpya kwa CAG ikionesha kuwepo kwa marekebisho ya takwimu za makusanyo ya Mfuko Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Oktoba mwaka jana akitoa kauli ya serikali bungeni siku kuhusu hoja ya zilipo fedha hizo Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango alidai kuwa, kati ya fedha hizo Sh. bilioni 697.9 zilitumika kulipa hati fungani, Sh. bilioni 689.3 ni mapato tarajiwa na Sh. bilioni 203.9 mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Alieleza kuwa, katika uandishi wa taarifa ya CAG, kulitumika taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti na kwamba, hadi Juni 2017 mapato yaliyokusanywa yalikuwa Sh. trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa Sh. trilioni 23.79.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh. bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za serikali zilizoiva,” Dk. Kijaji alisema na kuongeza:

“Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika, hivyo basi baada ya kufanya uhamisho, jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi (exchequer issues) yalikuwa Sh. trilioni 24.4.”

Alisema kuwa, katika kipindi cha mwaka wa 2012/2013 hadi 2016/2017, serikali ilikuwa katika kipindi cha mpito cha kutekeleza mpango mkakati wa kuandaa mapato ya serikali kwa kutumia viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (International Public Sector Accounting Standards (IPSAS Accrual).

Na kwamba katika kipindi hicho, serikali ilitumia mfumo huo kukusanya hesabu za mapato na matumizi ya serikali kuiwezesha kikamilifu kutambua hesabu za mali, madeni na makusanyo ya kodi.

Alisema, hakuna kiasi cha Sh. trilioni 1.5 kilichopotea au kutumika bila kuidhinishwa na Bunge, bali ni kutokana na serikali kutumia mfumo wa IPSAS Accrual.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!