July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la sukari: Mkapa alipuliwa

Spread the love

MBUNGE wa Moshi Vijijini, Anthony Komu, amemtuhumu Rais John Pombe Magufuli, kusababisha uhaba wa sukari nchini, anaandika Josephat Isango.

Anasema, uamuzi wa rais wa kupiga marufuku uigizaji wa sukari kutoka nje, ndiyo chanzo cha kuwapo kwa uhaba mkuwa wa bidhaa hiyo nchini na kuonya kuwa “kuna hatari ya uchumi kuvurugika.”

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge mjini Dodoma, Komu alisema “Rais Magufuli anataka kudanganya umma, kwamba kilichosababisha sukari kuadimika kwa sukari, ni hatua ya baadhi ya wafanyabiashara kuficha sukari.”

“Hapana. Kilichosababisha uhaba wa sukari, ni tangazo la rais la kupiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje; tangazo ambalo halikuzingatia mahitaji halisi ya ndani na uwezo wa uzalishaji viwanda vyetu.”

Komu ambaye ni waziri kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, amedai kuwa mahitaji ya sukari kwa mwaka ni tani 590, wakati uwezo wa viwanda vya ndani, ni kuzalisha tani 300,000 (laki tatu).

Akiongea kwa kujiamini Komu alisema, kwa utafiti wake, Rais Magufuli atakuwa ameshauriwa vibaya na baadhi ya wanasiasa wenye maslahi katika biashara ya sukari nchini.

Anasema, “…kwa maoni yangu, Rais Magufuli amepata ushauri mbaya kutoka kwa rais mstaafu Benjamin Mkapa. Vinginevyo, kusingekuwa na marufuku ya kuingiza sukari kwa sababu ya kulinda viwnada vya ndani.”

Kwa mujibu wa Komu, rais huyo mstaafu wa awamu ya tatu – Benjamin Mkapa – ni mmoja wamiliki wa mashamba ya miwa yaliyoko Mtibwa.

“Nchi hii ina viwnada vingi mno. Kwa nini Magufuli alinde viwanda vya sukari pekee yake na kuacha kulinda viwanda vingine? Bila shaka ni kwa sababu, Mzee Mkapa ambaye ni mmoja wa maswahiba wakubwa wa Magufuli, ni mmoja wa wamiliki wa sukari,” ameeleza.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Komu alikuwa ameongozana na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, aliyedai kuwa ana ushahidi kuhusika kwa Mkapa na kuwapo kwa tatizo la sukari nchini.

“Huyu Mkapa siyo tu mkulima wa miwa, bali anatajwa kuwa mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha Sukari cha Mtibwa. Hivyo ametumia urafiki wake na Rais Magufuli, kukinifaisha binafsi,” ameeleza Kubenea.

Amesema tatizo la uhaba wa sukari linajulikana kila mwaka nchini, lakini serikali kwa makusudi au kwa kuzembea, imeshindwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo.

Alidai kuwa tatizo la uhaba wa sukari nchini litaathiri kwa kiwango kikubwa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Amesema, kwa kawaida katika mfungo wa Ramadhani, matumizi ya sukari huwa makubwa kulinganisha na siku za kawaida.

error: Content is protected !!