NI kama vile sakata la Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad ndio kwanza linaanza baada ya kuvuka mipaka ya nchi. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Tayari Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA), maspika wanachama wa bunge hilo pamoja na wanasheria wakuu wa Nchi Jumuiya za Madola wamearifiwa juu ya kile kinachoelezwa mkanganyiko wa mipaka ya kimalaka kati ya Taasisi ya Bunge la Jamhuri na Ofisi ya CAG nchini Tanzania.
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini siku mbili zilizopita alimwandikia mkuu wa CPA, Akbar Khan kumweleza hatua iliyochukuliwa na Spika Ndugai kuwa, ni kinyume na Katiba ya Nchini lakini pia inaingilia mamlaka nyingine.
Kwenye andishi lake hilo Zitto ameeleza kwamba, iwapo Prof. Assad atahojiwa, basi Katiba ya Tanzania itakuwa imekiukwa waziwazi.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo ameieleza CPA, chanzo cha Ndugai kumtaka Prof. Assad kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge tarehe 21 Januari 2019 kujibu “tuhuma za kudhalilisha Bunge” ni kutokana na maoni yake binafsi kama Mtanzania.
Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo ameeleza kuwa, wito wa Ndugai si tu umevunja Katiba ya Nchi, lakini pia unaweza kuwa hatari zaidi kwenye jumuiya.
Na kwamba, iwapo agizo la Spika Ndugai litaitikiwa, basi makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2013 juu ya uhuru wa taasisi ya ukaguzi, yatakuwa yamevunjwa.
Wiki iliyopita akiwa Marekani, Prof. Assad alizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Kituo cha Umoja wa Kimataifa akisema kwamba, mhimili huo wa kutunga sheria, umekuwa dhaifu mno na hivyo umeshindwa kutimiza wajibu wake.
Kutokana na kauli hiyo, mbele ya waandishi wa habari Ndugai alisema“…ninamtaka CAG, kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa hiari yake, tarehe 21 Januari mwaka huu. Vinginevyo, nitaagiza akamatwe na kuletwa mbele ya kamati kwa pingu.”
Hatua ya Zitto kumwandikia barua hiyo Khan imemsukuma Spika Ndugai naye kuandika barua kwenda kwa jumuiya hiyo akieleza kuwa, kilichofanywa na taasisi yake hakijakiuka mamalaka ya kikatiba. Barua hiyo iliandikwa jana Alhamisi.
Ndugai ameeleza kuwa, suala la CAG kuitwa kuhojiwa halijawahi kutokea popote na kuongeza kuwa, haijawahi kutokea kwa CAG kuita muhimili wa bunge kuwa ni dhaifu na kwamba, taarifa ya Zitto kwa CPA imepindishwa. Hata hivyo amesema, CPA haina uwezo wa kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Hivi karibuni akijibu kwamba kama ataitikia wito wa Spika Ndugai, Prof. Assad alisema, “…sasa kwa kuheshimu katiba yetu na kwa kuwa sitaki kuwa miongoni mwa waivunjao katiba, niseme hivi, Ibara ya 18 (a) inampa kila mtu uhuru wa kutoa maoni.
Tayari Spika Ndugai ameeleza kuwa, ofisi yake imeandaa barua kwenda kwa CAG, kwa ajili ya kumwita kwenye kamati hiyo tarehe 21 Januari 2019.
Leave a comment