January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Nabii Mwingira pasua kichwa, Polisi yasema…

Askofu wa Kanisa la Efatha, Josephat Mwingira

Spread the love

 

SAKATA la Kiongozi wa Kanisa la Efatha nchini Tanzania, Mtume na Nabii Josephat Mwingira limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kushikwa kigugumizi kutoa taarifa ya kinachoendelea kama ilivyoahidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Nabii Mwingira anatuhumiwa kutoa tuhuma nzito za kunusurika kuuawa mara tatu na watu wa serikali jambo lililomfanya Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene kuagiza Polisi Dar es Salaam kumtafuta na kumhoji.

Waziri Simbachawene alitoa agizo hilo Jumatatu ya tarehe 27 Desemba 2021 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akisema, kwa kuwa kiongozi huyo wa dini ametolewa tuhuma hizo akiwa Dar es Salaam “RPC wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, amtafute ili tuweze kupata maelezo yake zaidi.”

Mara baada ya taarifa hiyo, jioni ya siku hiyohiyo, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro naye alitoa taarifa kwa umma akimtaka Nabii Mwingira kujisalimisha ndani ya saa 24 ili kuweza kuhojiwa.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime

Juzi jioni Jumatano, ikiwa ni saa 24 zilizotolewa kumalizika, MwanaHALISI Online lilimtafuta Kamanda Muliro kwa simu kujua kinachoendelea kuhusu sakata hilo ambapo alisema, “tutatoa taarifa kesho (jana) na kwa sasa tuacheni tuendelee na uchungizi wetu.”

Hata hivyo, jana Alhamisi, tarehe 30 Desemba 2021, MwanaHALISI Online lilimtafuta kwa mara nyingine Kamanda Muliro kama alivyoahidi kutoa taarifa ambapo alisema, “mpigie msemaji wa jeshi la polisi.”

Alipoelezwa agizo la Waziri Simbachawene lilikuwa kwa jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Muliro alisema, “wewe mpigie msemaji wa jeshi David Misime, si namba yake unayo.”

Mwandishi alimuuliza suala hilo limetoka ngazi ya kanda maalum na kwenda juu, Kamanda Muliro alijibu, “mimi sijasema limetoka kwenye level, hiyo ni tafasiri ni yako. Na mimi sitaki kujadili agizo na wewe si unachokitaka ni habari, mpigie afande wangu Misime ili tusiwe wasemaji wengi.”

MwaanHALISI TV linaendelea kumtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.

error: Content is protected !!