August 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Moto K/koo: Chadema wataka Majaliwa, Simbachawene wajiuzulu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua soko la Kariakoo lililoungua moto jana jioni

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  Kanda ya Pwani, kimemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ajiuzulu kwa kushindwa kudhibiti maafa katika tukio la moto uliounguza Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wengine waliotakiwa kujiuzulu kufuatia sakata hilo ni , Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene na  Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, John Masunga.

Wito huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 13 Julai 2021, mkoani Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Baraka Mwago, baada ya kutembelea soko hilo, jana tarehe 12 Julai mwaka huu.

Moto huo ulianza kuwaka usiku wa Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021. Serikali imeunda tume ya kuchunguza chanzo cha moto huo, ambayo inatarajia kutoa taarifa yake Jumapili tarehe 18 Julai mwaka huu.

Mwago amesema kuwa, viongozi hao wanapaswa kuwajibika kutokana na kushindwa kusimamia vyema taasisi zilizo chini yao, zinazoshuhulikia masuala ya majanga nchini.

“Kamishna Jenerali wa zimamoto,  waziri wa mambo ya ndani hata waziri mkuu wanapaswa kujiuzulu. Sababu katika ofisi ya waziri mkuu   kuna kitengo cha maafa lakini kila siku taarifa zile zile, mzee wangu Kasim Majaliwa apishe labda aletwe mwingine ambaye ataweza kusimamia kitengo hicho,” amesema Mwago.

Mwago ameongeza “kuna sababu gani hawa watu kuwa ofisini? Lazima tutengeneze utaratibu watu kuwajibika. Kama hili linafanyika katika soko kuu lakini wanaendelea na nafasi zao. Tunawasihi  waone sababu ya kuona aibu. Tuombe mtupishe na muondoke.”

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, Simbachawene alitakiwa kujua utendaji wa jeshi la zimamoto, badala ya kuuliza maswali juu ya changamoto za jeshi hilo, ambayo yalipaswa kuulizwa na wananchi.

“Waziri Simbachawene anatoa maneno ya kukinzana, yeye ndiye anayesimamia kikosi cha kuzima moto anatuhoji. Hili jambo ilitakiwa tuulize sisi ambao hatuna mamlaka hayo. Na bado anaendelea kuwa ofisini na wala hajashtuka,” amesema Mwago.

Jana, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Temeke, Bakari Mrisho, alitaja changamoto zilizosababisha  jeshi hilo kuchelewa kuuzima moto huo,  ikiwemo mabomba ya maji ya kuzimia moto (Fire Hydrants), kushindwa kufanya kazi kutokana na kuwa na kasi ndogo ya utoaji maji.

Changamoto nyingine iliyokwamisha zoezi hilo, ni baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu kwenda katika eneo la tukio kwa ajili ya kufanya uhalifu.

Pamoja na changamoto ya mrundikano wa bidhaa za wafanyabiashara barabarani, hali iliyochelewesha magari ya zimamoto kupita.

error: Content is protected !!