May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la mahindi: Tanzania yaionya Kenya

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeitaka Kenya kuacha upotoshaji kwamba mahindi ya Tanzania hayafai kwa matumizi ya binadamu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tanzania imeishauri Kenya kutumia njia sahihi kufikisha malalamiko yake, tofauti na kile inachofanya sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Hussein Bashe, Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania tarehe 8 Machi 2021, wakati akielezea msuguano unaoendelea kati ya Tanzania na Kenya.

Mazungumzo hayo, yanalenga kumaliza mkwamo wa mahindi kutoka Tanzania yaliyozuiwa kuingia Kenya kupitia mpaka wa Namanga, Arusha.

Mahindi hayo yalizuiwa kuanzia tarehe 5 Machi 2021, baada ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini humo, kupiga marufuku mahindi ya Tanzania na Uganda kwa madi ya kutokukidhi viwango vya usalama wa chakula cha binadamu.

Bashe ametoa maelezo ya kinachoendelea kuhusu sakata hilo, kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba.

“Salaam ndg zangu, nataka niseme kuwa mahindi ya Tanzania ni salama kwa matumizi ya binadaam na wanyama na yanakidhi vigezo vyote vya kikanda na kimataifa.

“Biashara ni suala la hiari, wanaweza kununua au kutonunua kutoka kwetu. Kinachotusumbua sisi ni kauli ya upotoshaji ya wizara ya kilimo ya Kenya. Sisi Tanzania tunafanya biashara ya mahindi na mataifa na taasisi za kimataifa na inaendelea,” amesema

Naibu waziri huyo amesema, wanaendelea na mazungumzo kama wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) “ili kufikia maelewano ya kuheshimiana.”

“Hata sampuli walizochukua Shirika la Viwango la Kenya (KEBS) katika mpaka wa Horohoro siku ya Jumamosi, matokeo hayakua kama ambavyo Kenya walivyohubiria Dunia. Tunawasihi wenzetu, jirani zetu na ndugu zetu Kenya watumie njia sahihi za malalamiko,” amesema.

Amesema, Tanzania inaendelea kuuza mahindi maeneo mengine kama DRC, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini huku Shirika la Chakula Duniani (WFP) likiendelea kununua mahindi hayo.

“WFP inanunua mahindi na kesho (leo), kupitia Bandari ya Kasanga Mkoa wa Rukwa, watapakia meli yenye tani 300 za mahindi kuelekea Bujumbura, Burundi. Mahindi yetu ni salama.

“Tunasisitiza kuwa, Afflatoxine levels na Moisture level ya mahindi ya Tanzania ambayo tunatumia ndani na tunayouza nje yanakidhi vigezo vya kimataifa, tusiwe na hofu tunafanya majadiliano kufikia muafaka utakao jenga kuheshimiana,” amesema Bashe.

Amesema “ni dhahiri kuwa EAC inafahamu ni nchi gani inaongoza kwa sumukuvu. Ieleweke biashara ni hiari lakini upotoshaji hautavumilika.

“Tutaendelea kufata njia za kidiplomasia kumaliza jambo hili. Tunalichukulia kwa uzito unao stahili ni wajibu wetu kutetea maslahi ya Watanzania,” amesema.

error: Content is protected !!