October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Lugola: Kiza kinene chatawala, DPP aliweka kiporo

Spread the love

KIZA kinene kimetawala katika ufujaji wa mabilioni ya shilingi yaliyotaka kutumika katika mkataba tata wa ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania (JZU), kufuatia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, kushindwa kuweka wazi, ni lini hasa, watuhumiwa watafikishwa mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Miongoni mwa wanaotuhumiwa katika kashifa hiyo, ni pamoja na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Kangi Lugola na wenzake 16, akiwamo aliyekuwa Kamishena wa jeshi hilo, Thobias Andengenye.

Ununuzi wa vifaa vya jeshi la Zimamoto ambao ulifanyika bila kufuata taratibu za manununi na sheria nyingine za nchi, umeligharimu taifa, zaidi ya Sh. 1 trilioni.

Kufahamika kuwapo kwa mkataba huo, kulielezwa kwa mara ya kwanza na Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, tarehe 23 Januari mwaka huu.

Rais Magufulialitoa tuhuma hizo katika hafla ya makabidhiano ya nyumba za maafisa na askari wa jeshi la Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo wa nchi alisema, mkataba huo wa ununuzi wa vifaa vya jeshi la Zimamoto, haukupangwa kwenye Bajeti Kuu ya Serikali, na wala haukupitishwa na Bunge, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Kufutia tuhuma hizo, Rais Magufuli, alimfuta kazi – hapo hapo – Lugola na Andengenye. Akamteuua George Simbachawene, kumrithi Lugola na John William Masunga, ambaye alikuwa Naibu Kamishena wa Jeshi la Magereza, kumrithi Andengenye.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Brigedia Jenerali, John Mbungo, aliwambia waandishi wa habari, tarehe 22 Februari 2020, kwamba jalada la uchunguzi lililosheheni tuhuma dhidi ya Lugola na wenzake, anatarajia kulifikisha kwa DPP, Mganga haraka iwezekanavyo.

Alisema, ofisi yake imekamilisha uchunguzi wa suala hilo kwa zaidi ya asilimia 99, na kubaini kuwa suala hilo linahusiana na uhujumu uchumi na hivyo, kuamua kulipeleka jalada hilo kwa DPP kwa hatua zaidi za kisheria.

Lakini Biswalo alipoulizwa na wanahabari kama ofisi yake imepokea jalada hilo, alisema “muda muafaka ukifika, nitalizungumzia suala hilo.”

DPP Biswalo alitoa kauli hiyo ikiwa ni takribani siku 20 zimepita, tangu Mbungo aliposema anatarajia kulifikisha jalada la uchunguzi kuhusu sakata hilo, katika ofisi yake.

Leo Jumanne, tarehe 26 Mei 2020, ikiwa imetimia siku 94, tangu TAKUKURU kueleza kuwa uchunguzi wa suala hilo umekamilika na jalada la kesi litapelekwa kwa DPP, MwanaHALISI Online, imeshindwa kupata kwa ufasaha, kinachoendelea kwenye kesi hiyo, baada ya Biswalo kueleza kwa njia ya simu, “kuna taratibu za kiofisi zinashughulikiwa.”

Alisema, “sifanyi kazi kwenye mitandao, kuna taratibu za kiofisi za kushughulikia mambo,” ameeleza na kisha kukata simu.

error: Content is protected !!