August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Loliondo – Amnesty International wamuandikia barua nzito Samia

Spread the love

SHIRIKA la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limemuandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan, kutaka kusitishwa kwa oparesheni ya kuweka alama za mipaka na wamasai 25 waliokamatwa kutokana na madai kufanya vurugu katika zoezi hilo kwenye eneo Loliondo katika mbuga ya Taifa ya Serengeti mkoani Arusha, waachiwe huru mara moja.

Katika barua hiyo iliyoandikwa tarehe 13 Julai, mwaka huu Shirika la Amnesty International limemsihi Rais Samia kutoa maagizo ya kuacha mara moja kuendeleza eneo hilo hadi wamaasai watakapopewa elimu ya kutosha kuhusu zoezi hilo na walioingia kwenye eneo hilo la pori tengefu lenye kilomita za mraba 1500, waondoke kwa hiyari. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katibu Mkuu Amnesty International, Agne’s Callamard

Pia limetaka uchunguzi huru na wa kina ufanyike kuhusu makabiliano yaliyotokea kati ya maofisa wa usalama na wamaasai tarehe 9 Juni, mwaka huu.

Aidha, katika barua hiyo ambayo ipo kwenye tovuti yao, Amnesty International wamesema kwamba watu 25 wanazuiliwa na polisi kwa kupinga zoezi la serikali la kuweka alama hizo za mipaka kwa kuhisi kuwa wapo hatarini kuondolewa katika ardhi yao ambayo wameishi kwa miaka mingi.

Limeongeza maofisa wa polisi walitumia nguvu katika kuwatawanya wamaasai waliokuwa wakiandamana kwa amani kupinga hatua ya maofisa wa usalama kusimamia zoezi hilo.

MAJINA YA WATU WALIOKAMATWA

Shirika la Amnesty International limesema kwamba lina ushahidi kwamba watu wafuatao wanazuiliwa na polisi: Molongo Daniel Paschal, Albert Kiseya Selembo, Simeli Parmwati, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati Sirikoti, Ingoi Olkedenyi Kanjwel na Sangau Morongeti Ngiminiso.

Wengine ni Morijoi Ngoisa Parmati, Morongeti Meeki Masako, Kamabatai Lulu, Moloimeti Yohana Saing’EU, Ndirango Senge Laisier, Joel Clemes Lessonu, Simon Naiam Orosikiria, Damiani Rago Laiza, Mathew Kursas Njausi, Taleng’o Twambei Leshoko, Kijoolu Kakenya Olojiloji, Shengena Joseph Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Lekerenga, Fred Victor, Wilson Tiuwa Kilong, James Memusi Taki na wengine 5 ambao majina yao hayajatajwa.

Katika barua hiyo, shirika hilo limesema ripoti za walioshuhudia tukio la tarehe 9 Juni, mwaka huu zinasema kwamba polisi na walinzi wa mbuga waliwashambulia wamaasai kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi. Watu kadhaa walijeruhiwa na mtu mmoja (polisi) kufariki.

Limesema wamaasai wengi walikimbilia nchi jirani ya Kenya kwa matibabu, waliokamatwa walifunguliwa mashtaka kabla ya makosa kufanyika.

Barua hiyo inasema kwamba “walikamatwa hata kabla ya polisi huyo kuuawa na mashtaka yalibadilishwa mara nne na kupandikiziwa kesi ya kupanga kumuua polisi na kuongeza majina ya watu wengine kwenye orodha ya watu wanaozuiliwa na polisi.”

MZOZO KATI YA WAMAASAI NA SERIKALI

Kwa mujibu wa serikali, kuna umuhimu mkubwa wa kuhifadhi mazingira dhidi ya uharibifu unaofanywa na jamii ya wamaasai ambao ni wafugaji, katika mbuga ya kitaifa ya Serengeti.

Barua iliyoandikwa na Amnesty International kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa sababu hiyo, serikali inawaondoa watu kutoka eneo la kilomita 1500 za mraba katika divisheni ya Loliondo na sehemu za Ngorongoro na kuwaachia eneo la zaidi ya kilomita 2500 kwa ajili ya shughuli za kibinadamu

Msemaji wa serikali, Gerson Msigwa aliiambia Sauti ya Amerika kwamba “inachofanya serikali ni kulinda mazingira ni jukumu la kila serikali kufanya hivyo. Watu hao wanatoka kwa hiari bila kushurutishwa.”

Kwa mujibu wa Amnesty, operesheni ya sasa ya kuwaondoa wamaasai ni jaribio la nne katika mzozo wa ardhi hiyo ambao umechukua zaidi ya muongo mzima.

Maofisa wa usalama waliwahi kujaribu kuwatimua wamasai kutoka ardhi hiyo miaka ya 2009, 2013 na 2017. Operesheni ilifanyika katika vijiji vinne vya Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arash.

Mahakama ya jumuiya ya Afrika Mashariki ilitoa agizo kwa serikali kuacha operesheni hiyo, tarehe 26 Septemba, 2018. Agizo hilo lilisitisha shughuli hiyo ya serikali “hadi uamuzi kamili utakapotolewa.”

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa na jamii ya wamaasai, ilipangwa kwamba uamuzi kamili wa mahakama ulikuwa umetarajiwa kutolewa tarehe 22 Juni mwaka huu lakini mahakama hiyo iliahirisha hadi Septemba 2022.

MSIMAMO WA SERIKALI

Aidha, Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa aliiambia Sauti ya Amerika, katika kipindi cha Kwa Undani kwamba “hakuna zuio lolote lililofanywa dhidi ya serikali kuendelea kufanya shughuli za serikali. Kinachofanyika Loliondo ni kuweka alama, na ni moja ya majukumu ya uhifadhi kuwaonyesha watu eneo linalopaswa kutumiwa na wananchi ni hili, na eneo hili limehifadhiwa.

“Umuhimu wa eneo la kilomita za mraba 1500 lililopo pale Loliondo ni kubwa na lenye maslahi ya taifa. Pale ndipo mahali kuna vyanzo vya maji vinavyohudumia hifadhi zetu nyingi zikiwemo Ngorongoro, Serengeti, Meyatu na mapori ya akiba,” alisema.

Msigwa alisisitiza kwamba “Hakuna taasisi ambayo inaweza ikaja ikaiamuru Tanzania kwamba usifanye kitu fulani… hatufanyi hivyo. Kama kuna shirika lina maoni au limefanya utafiti, utaratibu ni kwamba wanawasilisha maoni na utafiti wao kwa serikali. Haliwezi likaja na kuiamrisha nchi ya Tanzania. Hii ni nchi huru. Huwezi kutuamrisha. Huo utaratibu haupo.”

error: Content is protected !!