July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Lipumba latikisa bunge

Wabunge wa UKAWA wakisimama wakipinga kukataliwa kujadiliwa hoja ya kupigwa na Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

SAKATA la kukamatwa, kupigwa na kufunguliwa shitaka la uchochezi kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, limezidi kutikisa bunge. Anaripoti Pendo Omary.

Leo, Bunge limejadili hoja iliyotolewa jana na Mbunge mteuliwa na Rais, James Mbatia (NCCR Mageuzi) kuhusu kutaka bunge kusitisha shughuli zake za kawaida na kujadili tukio hilo ambalo ni la dharura kwa sababu linahusu usalama wa wananchi na ukandamizaji wa haki za wananchi.”

Hoja hiyo imejadiliwa baada ya Spika Anna Makinda, kuahirisha ghafla shughuli za bunge kufuatia mvutano mkali uliotokea alipokuwa akijibu kwamba serikali ipewe muda wa kujiandaa kuwasilisha taarifa yake kesho yake, yaani leo.

Spika Makinda alipoanzisha mjadala leo, alianza kwa kumuita Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe atoe taarifa rasmi ya serikali; alisema polisi walichukua hatua baada ya viongozi wa CUF kukataa amri halali ya kutakiwa kutofanya maandamano wala mkuano wa hadhara.

Wabunge wa Kambi ya Upinzani, hasa watokao vyama vitatu vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambavyo ndivyo vyenye wabunge, walitiririka kuchangia na kupinga msimamo huo wa serikali.

Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), Joshua Nassari (Chadema), Khatibu Rajab (CUF), walishiriki. Aliyeanza alikuwa Mohamed Habibu Mnyaa (CUF), aliyesema utendaji wa Jeshi la Polisi umekuwa usiojenga urafiki wa kikazi na raia.

Mnyaa wa jimbo la Mkanyageni, alisema katika tukio la juzi Polisi walipokuwa wakipiga waandamanaji wa CUF, walitumia spana ya gari kumpiga kichwani Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Umma, Abdallah Kambaya, aliyekuwa amefuatana na Prof. Lipumba.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe huku akionesha nyaraka, amesema upinzani wamekuwa wakitoa malalamiko ushahidi wa namna Jeshi la Polisi linavyotumia nguvu kubwa katika utendaji wao na hivyo “kutesa na kuua raia pamoja na wanasiasa wa upinzani lakini serikali haichukui hatua.”

“Tumekuwa tukiomba ziundwe tume za uchunguzi za kimahakama kushughulikia malalamiko haya, lakini serikali imekuwa ikipuuza,” alisema Mbowe huku akimtaja Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa akiongoza kutosimamia utendaji wa haki.

Wabunge wa CCM waliochangia mwisho katika hoja, walitoa maelezo yaliyojenga taswira ya kukingia kifua maovu, japo baadhi yao walikuwa wakitaka kuonekana kama wanaopinga maovu.

Yahya Kassim Issa (Chwaka), Sadifa Juma Khamis (Donge) na Livingstone Lusinde (Mtyera) walisema Prof. Lipumba aliguswa tu wala hakupigwa, “angepigwa asingeweza kutembea.”

Lusinde anayejulikana kwa kutoa kejeli dhidi ya masuala muhimu yenye maslahi ya taifa, alisema kwa mara ya kwanza Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri kwa sababu limemshughulikia kiongozi wa waandamanaji.

Mbatia alipoitwa kufanya majumuisho ya hoja, alisema kila mtu analipenda ziwa la mama yake, lakini ni aibu kukuta polisi wanampiga mwanamama kwenye ziwa lake huku akiwa ameshadhibitiwa.

Aliita kitendo hicho ni ugaidi uliopitiliza mpaka na ipo haja ya kutazamwa upya sheria za jeshi hilo ili liwe rafiki kwa raia badala ya kuwachukiza na kukataa kushirikiana nalo hata kuamua nao kuwapiga polisi.

“Hiki ni kitendo cha kigaidi… Suala la jinai linaendelea. Ukifanya jinai leo, miaka 10 au 20 ijayo jinai haitafutika. Leo unashabikia mauaji, kesho hautokuwepo,” amesema Mbatia.

Lipumba alikamatwa na kupigwa na Polisi wakati wakiwa wanasambaratisha wana-CUF, eneo la Temeke Mwisho kiongozi huyo alipokuwa anaenda Mbagala Zakhem kukutana na waandamani ili kuwapa taarifa ya kuzuiwa kwa maandamano ya amani na mkutano.

Maandamano na mkutano yaliandaliwa kama sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 14 ya mauaji ya wafuasi wapatao 70 wa chama hicho waliokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2000 Zanzibar. Polisi na vyombo vingine walifanya hivyo walipokuwa wakiyavunja maandamano hayo Januari 27, 2001.

error: Content is protected !!