LICHA ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kukiri kumshikilia Tito Magoti, Ofisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), haijulikana mahala alipo mwanaharakati huyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Leo tarehe 21 Desemba 2019 jijini Dar es Salaam, Familia ya Tito pamoja na LHRC wamewaeleza wanahabari kwamba, hawafahamu Kituo cha Polisi anaposhikiliwa mwanaharakati huyo.
Wakili Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, amesema baada ya Kamanda Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana kukiri kuwa wanamshikilia Tito, wametembelea vituo vyote vya polisi, lakini hawakumkuta mwanaharakati huyo.
“Mpaka tunatoa tamko hili hatujui ni kituo gani cha polisi anachoshikiliwa ndugu Tito, vituo vyote vikubwa tulivyotembelea hakuna hata kituo kimoja kilichokiri kumshikilia, hata baada ya tamko la Kamanda Mambosasa, tulikwenda kituo cha kati hatukumkuta Tito,” ameeleza Wakili Henga.
Wakili Henga ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kueleza Tito anashikiliwa katika kituo gani cha polisi, pamoja na makosa anayotuhumiwa, ili waendelee na taratibu za kumuombea dhamana.
“Kama sehemu ya kuiondoa nchi yetu katika dosari ya kuonekana kutoheshimu haki za raia wake, tunaliomba Jeshi la Polisi kutaja kituo cha polisi kinachomshikilia Tito na kosa la jinai wanalomtuhumu nalo,” ameomba Wakili Henga.
Edward Magoti, Kaka wa Tito, akizungumza kwa niaba ya familia ya mwanaharakati huyo, wameliomba Jeshi la Polisi kueleza mahala alipo ndugu yao.
“Sisi tunaliomba Jeshi la Polisi kueleza mahali alipo ndugu yetu, sababu hatujui kituo gani anachoshikiliwa, badala yake polisi walikwenda nyumbani kwake kupekua,” amesema Edward.
Leave a comment