Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Sakata la kufukuzwa Chadema: Kishoa ajichanganya bungeni
Habari za SiasaTangulizi

Sakata la kufukuzwa Chadema: Kishoa ajichanganya bungeni

Jesca Kishoa
Spread the love

 

JESCA Kishoa, mbunge wa Viti Maalumu (asiyekuwa na chama), ameuthibitishia ulimwengu, kuwa kuwako kwake bungeni, ni kinyume na amefutwa uanachama katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora 2021/22, leo Ijumaa, Kishoa alisema, kuna shida kubwa ya utawala bora nchini.

Kishoa alikuwa akieleza kile alichoita, “athari ya marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, iliyotangazwa na serikali, miaka mitano iliyopita.”

Mwanasiasa huyo na wenzake 18, wamefukuzwa uanachama wa Chadema, tarehe 27 Novemba 2020, kufuatia kupatikana na hatia ya makosa ya utovu wa nidhamu, usaliti, kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro; na kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama.

Mashitaka mengine, ni pamoja na kughushi nyaraka za chama na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama chenyewe.

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha, Halima James Mdee; waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Katika orodha hiyo, wamo pia Hawa Subira Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar.

Mbali na viongozi hao wa Bawacha, Kamati Kuu ya chama hicho, iliyokutana jijini chini ya uenyekiti wa, Freeman Mbowe, iliwavua uanachama, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine waliofukuzwa Chadema, Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Kishoa na wenzake, wanaongozwa na Mdee, kukiri kufutwa uanachama wa chama hicho.

Hatua ya Kishoa kukiri kuwa siyo mwanachama wa Chadema, imethibitisha madai ya wengi, kuwa hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuendelea kuwang’ang’ania wabunge hao, ni kinyume na Katiba ya Jamhuri na sheria za nchi.

Akichangia mjadala huo bungeni, Kishoa alisema, yeye ni mhanga wa kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa na kwamba, amekutana na kadhia hiyo, wakati alipokuwa mwanachama wa Chadema.

Kabla ya kufukuzwa uanachama wa Chadema, Kishoa alikuwa naibu katibu mkuu wa Baraza la Wanawake taifa (Bawacha).

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalum

Alisema, “sitaki kubishana na kiti chako Naibu Spika (Tulia Ackson), niseme mimi ni mhanga kwenye mikutano ya vyama vya siasa. Nikiwa naibu katibu mkuu wa wanawake Chadema, kabla sijaondolewa kwenye chama changu, haya nilikutana nayo.”

Kabla hajamalizia maelezo yake hayo, Kishoa alikatishwa baada ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba kutoa taarifa, wakihoji mwanasiasa huyo ni mbunge wa chama gani huku wengine wakisikika wakisema, “kumbe alishafukuzwa.”

Baada ya wabunge wa CCM kuhoji uanachama wa Kishoa, Naibu Spika, Dk. Tulia aliingilia kati mjadala huo kwa kumtaka mwanasiasa huyo afute kauli yake, kwani ofisi ya spika ina taarifa rasmi zinazothibitisha kuwa yeye ni mwanachama wa Chadema.

Tulia alisema, “Kishoa hii kauli yako aidha uifute kwa sababu ofisi ya spika haina taarifa ya wewe kuondolewa kwenye chama chako, kama ungeondolewa kwenye chama chako usingekuwa humu ndani. Sababu walioko humu ndani wana vyama vya siasa.”

Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika

Naibu Spika huyo alisisitiza, “ndio katiba yetu inasema na ndio hiyo katiba unaitetea hapa, ile katiba hairuhusu mtu ambaye hana chama awepo humu ndani, Kishoa futa kauli yako.”

Kufuatia kauli hiyo ya Tulia ya kumtaka Kishoa afute kauli yake, mbunge huyo alisema “Mheshimiwa spika, hatujaondolewa kwenye chama, bado mimi ni mwanachama wa Chadema sababu tuko kwenye taratibu na tumekata rufaa. Taratibu zinaendelea.”

Baada ya Kishoa kusahihisha kauli yake hiyo, Dk. Tulia alisisitiza kwamba mbunge huyo ameingia bungeni akiwa mwanachama wa Chadema.

“Taarifa rasmi za bunge ni kumbukumbu zinakaa pale, umezungumza kabla ya sentensi yako ya sasa kwamba kabla hujaondolewa kwenye chama chako, futa kauli yako kwanza halafu umalizie mchango wako,” amesema.

Aliongeza, “sababu ndani ya bunge hili tutakuwa tunavunja katiba kuwa na wewe humu kama umeondolewa uanachama wako, na ofisi ya spika haina taarifa ya wewe kuondolewa uanachama ndio maana humo humu ndani.”

Baada ya mjadala huo kuibuka bungeni, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema, chama chake, kiliwasilisha barua juu ya maamuzi yake ya kuwafukuza uanachama Mdee na wenzake.

Mnyika amesema, “Niabu Spika amesema uongo bungeni. Ukweli ni kuwa barua ya kuwafukuza uanachama wasaliti 19 walioitwa wabunge wa Chadema tuliipeleka kwa Spika kwa dispatch, tarehe 1 Disemba 2020.

“Tukapeleka nakala kwa mara ya pili kwa DHL tarehe 19 Disemba 2020. Matakwa ya katiba yatekelezwe sasa,” ameandika Mnyika katika ukurasa wake wa Twitter.

Baadhi ya waliofukuzwa Chadema, wamewasilisha rufaa Baraza Kuu la taifa, kupinga uamuzi huo. Baraza la Kuu la Chadema bado halijakutana kujadili suala hilo.

1 Comment

  • Ni aibu tupu kwa Tulia ambaye ni profesa wa sheria kumbambikizia mbunge chama ambacho si chake. Mwenyewe anasema kafukuzwa na hata chama kinasema kimemfukuza. Sasa mtabishana naye na chama? Wote wawili wanakubaliana kuwa hana chama. Nyie mnagangania tu
    HESHIMUNI SHERIA NA KATIBA YA NCHI JAMANI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!