CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewasilisha ombi kwa mahakama kuu, masjala ya Dodoma, kuomba itoe amri kwa Jeshi la Polisi mkoani humo, kumfikisha mahakamani, Mratibu wa Uhamasishaji wa Baraza lake la Vijana (Bavicha), Twaha Mwaipaya anayeshikiliwa na Polisi tangu tarehe 30 Juni, 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, ombi hilo limewasilishwa leo Jumatatu, tarehe 4 Julai 2022, ambapo chama hicho kinaomba mahakama itoe amri Mwaipaya afikishwe mahakamani au aachwe kwa dhamana.
Mnyika amedai Mwaipaya anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma.
“Tayari Chadema imewasilisha habeas corpus leo mahakama kuu Dodoma, dhidi polisi kumshikilia Twaha Mwaipaya, kinyume cha sheria na kutaka apewe dhamana. Tunasubiri kupangiwa Jaji na kupewa summons. Mawakili wanaendelea na hatua nyingine,” ameandika Mnyika katika ukurasa wake wa Twitter.
Mwaipaya anashikiliwa na Jeshi la Polisi, tangu alipokamatwa Ijumaa iliyopita, akiwa mkoani Morogoro, alipokamatwa na Polisi akiwa njiani kurudi Dar es Salaam, akitokea mkoani Dodoma katika ziara ya kikazi.
Kwa mujibu wa Chadema, Mwaipaya anashikiliwa na Polisi, kwa tuhuma za makosa ya mtandaoni, anayodaiwa kufanya mkoani Dodoma.
Leave a comment