Spread the love

SAKATA la ukamilishwaji wa mchakato wa upatikanaji kati mpya, pamoja na mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro, vimeibuliwa kwenye mkutano wa 49 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, wa mapitio ya hali ya haki za binadamu duniani (UPR). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Masuala hayo yameibuliwa jana tarehe 23 Machi 2022, jijini Geneva Uswisi na Mratibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa wakati wa upitiwaji wa matokeo ya hali ya haki za binadamu nchini.

Akiwasilisha tamko la mapitio ya hali ya haki za Binadamu Tanzania katika kipindi cha miaka minne (2017 hadi 2021), Olengurumwa, amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inajitahidi kukuza, kuendeleza na kulinda haki za binadamu na demokrasia nchini humo.

“Tunashukuru na kutambua maendeleo ya haki za binadamu tunayoendelea kuyapata tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka mmoja uliopita, pamoja na dhamira njema ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, katika kukuza na kuendeleza haki za binadamu na demokrasia nchini,” amesema Olengurumwa.

Hata hivyo, Olengurumwa ameiomba Serikali ikamilishe mchakato wa upatikanaji katiba mpya, uliokwama tangu 2015.

“Wito kwao ni kuendeleza mapenzi hayo na kupanua dhamira hii njema katika maeneo mengine yahusuyo haki za binadamu na utawala wa kisheria. Ili kuyafanya maendeleo ya hivi karibuni yawe endelevu, tunatoa wito wa maboresho mapana ya mifumo ya kisheria, ikiwemo ukamilishwaji wa mchakato wa kutengeneza katiba mpya,” amesema Olengurumwa.

Mbali na maombi ya ukamilishwaji mchakato wa katiba mpya, Olengurumwa ameiomba Serikali ivifanyie mabadiliko ya vifungu vya sheia vinavyoathiri shughuli za asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu.

Ambazo ni Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Pia Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (kuhusu Maudhui ya Mtandaoni), Mabadiliko ya Sheria ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, pamoja na Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu na Haki za Msingi za Binadamu (BRADEA).

Katika hatua nyingine, Olengurumwa ameiomba Serikali isitishe mpango wake wa kuwaondoa kwa hiari wananchi waishio kwenye Hifadhi ya Ngorongoro, kwa ajili ya kudhibiti ongezeko la shughuli za kibinadamu.

“Tunaishauri serikali kwa msisitizo mkubwa isitishe mpango uliopo, wa kuwaondoa jamii asili ya wa Masai 70,000 kwenye ardhi yao ya asili iliyoko Tarafa ya Ngorongoro, pamoja na mpango wa kumega ardhi ya vijiji vya Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 Wilayani Ngorongoro,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema “tunasisitiza uwepo wa ushirikishwaji mpana wa jamii unaozingatia misingi ya haki za binadamu, katika mipango yote ya Serikali ihusuyo maeneo hayo yenye mgogoro Wilayani Ngorongoro na muhimu zaidi kuruhusu watetezi wa haki za binadamu Ngorongoro kufanya kazi zao kwa uhuru.”

Kuhusu mapitio ya hali ya haki za binadamu nchini, Olengurumwa ameiomba Serikali, iangalie upya msimamo wake kuhusu mapendekezo 67 yaliyitilewa na baraza hilo, ambayo haijayakubali. Ambapo Tanzania imekubali kutekeleza mapendekezo 187 huku 20 ikikubali kutekeleza kwa sehemu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *