Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sakata la ATCL: Mwigulu, Lema ‘wachapana’
Habari za SiasaTangulizi

Sakata la ATCL: Mwigulu, Lema ‘wachapana’

Spread the love

SAKATA la kushikiliwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania Limited (ATCL) nchini Afrika Kusini kwa amri ya mahakama, limechochea mvutano baina ya wabunge wawili vijana, Mwigulu Nchemba wa Iramba Magharibi na Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini. Anaripoti Regina Mkonde …(endelea).

Mvutano kati ya Mwigulu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Lema wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeibuka baada ya Lema kuiasa serikali kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa mawakili wa Tanzania, waliosimamia kesi iliyoleta matokeo ya kukamatwa ndege iliyonunuliwa baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, wasilaumiwe kuwa si wazalendo.

“Kwa hili la ndege yetu kukamatwa Afrika Kusini, uzalendo sio kulaumu mawakili Watanzania waliopewa kazi, bali ni kumuonea huruma Mzee wa Kizungu juu ya deni analodai, njia sahihi ya kuthibitisha uzalendo ni kuwa na upendo na watu wote hata wasiokuwa damu yako,” ameandika Lema.

Kauli hiyo imemuibua Mwigulu ambaye amehusisha tukio hilo na vita vya kiuchumi kama apendavyo kusema Rais Magufuli, huku akisai ni ajabu kama kuna Mtanzania anashabikia kukamatwa ndege ya serikali.

“Tuko kwenye vita vya kiuchu; vya kibiashara. Ni ajabu sana kama kuna Mtanzania anashabikia ndege kukamatwa. Mtoto mpumbavu huona mali za baba yake si zake, ila baba aondokapo hugombania urithi, na akirithi hutapanya mali hiyo,” ameandika Mwigulu.

Tarehe 23 Agosti 2019, serikali kupitia Leonard Chamuriho, Katibu Mkuu Uchukuzi, alitoa taarifa ya kushikiliwa kwa ndege aina ya Airbus A220-300 kwa sababu ya amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Siku mbili baadae, Dk. Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali alisema ndege hiyo imeshikiliwa kutokana na kesi ya madai ya muda mrefu ya fidia ya ardhi iliyotwaliwa tangu miaka ya 1980 na kwamba madai ya ndege hiyo kuzuiliwa kwa sababu ATCL inadaiwa si ya kweli.

Dk. Abbasi alisema wanasheria wa serikali wanafuatilia kesi hiyo inayosemekana ilifunguliwa na Hermanus Steyn dhidi ya serikali ya Tanzania akidai malipo yake.

Hatua ya kukamatwa kwa ndege hiyo ambayo ni moja wapo ya ndege kadhaa zilizonunuliwa tangu Rais Magufuli alipoingia katika kulifufua shirika la ndege Tanzania, imesababisha mgawanyiko wa maoni ya wananchi wakiwepo wanaoshangilia kwa msimamo kuwa rais amekuwa akijisifia mno.

kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja miaka miwili baada ya ndege nyingine ya shirika hilo aina ya Bombedier kukamatwa nchini Canada, Julai mwaka 2017.

Ndege hiyo ilikamatwa kwa madai ya serikali kudaiwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Limited (SCEL), iliyokuwa ikijenga barabara kati ya Wazo jijini Dar es Salaam na Bagamoyo, mkoani Pwani.

Serikali iliingia kwenye mgogoro na kampuni hii, kufuatia uamuzi wake wa kuvunja mkataba huo; jambo ambalo lilisababisha SCEL kwenda mahakamani nchini Uingereza.

Katika maamuzi yake, tarehe 10 Juni mwaka 2010, mahakama ya usuluhishi ya migogoro ya kibiashara (ICSID), iliamuru serikali ya Tanzania kulipa kiasi cha Dola za Marekani 21 milioni.

Serikali haikulipa deni hilo; mpaka ndege ilipokamatwa nchini Canada, ilikuwa inapaswa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 38.1 milioni (Sh. 70 bilioni).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!