Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Sakata kufungiwa Mawio, MwanaHALISI lafika kwa waziri mkuu, yeye ajibu
Habari MchanganyikoTangulizi

Sakata kufungiwa Mawio, MwanaHALISI lafika kwa waziri mkuu, yeye ajibu

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu,
Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kasim Majaliwa, ameombwa kusaidi Idara ya Habari Maelezo kuhakikisha inatenda haki kwa Magazeti yaliyofungiwa ikiwemo Mawio na MwanaHALISI. Anaripoti Yusuph Katimba, Morogoro … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi, tarehe 20 Mei 2021 na Deodatus Balile, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), katika mkutano mkuu wa jukwaa hilo.

Magazeti yaliyofungiwa ni; Mawio, Tanzania Daima, MwanaHALISI na Mseto.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Magazeti ya Mawio na MwanaHALISI, licha ya kushinda kesi zao, bado Idara ya Habari Maelezo, imekataa kuwapa leseni, tunaomba usaidie hilo kwa kuwa lipo katika uwezo wako,” amesema Balile wakati akisoma risala ya jukwaa hilo.

Hata hivyo, Majaliwa akijibu hoja hiyo, amekiri kufungiwa kwa magazeti hayo manne na kusema, “sisi kama Taifa, tukijilinganisha na mataifa mengine, Tanzania inaongoza kwa kuwa na vyombo vingi vya habari, tunazo TV na redio nyingi na sasa tuna redio zimefikia 198 nchini, vituo vya TV 45 na magazeti hadi 257 yaliysajiliwa hadi sasa.”

Majaliwa amesema “tunachofurahi hadi sasa, hatuna redio hata moja imefungiwa, isipokuwa Wasafi TV walifungiwa, lakini walirejea. Magazeti yaliyofungiwa ni manne; Mawio, Mseto, MwanaHALISI na Tanzania Daima.”

“Jitihada zinaendelea kufanyika ndani ya serikali, ili na wao waweze kurejea kuendelea na shughuli zao. Kwa vile vilivyofungiwa kwa mujibu wa sheria, taratibu zitafuatwa kwa maelekezo ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan, ili nawao waweze kuondokana na makosa yao ili viweze kufanya kazi. Hii ndiyo nia njema ya serikali yetu,” amesema Majaliwa

Tarehe 6 Aprili 2021, Rais Samia, mara baada ya kumaliza kuwaapisha makatibu, manaibu katibu wakuu na viongozi wa taasisi za umma, Ikulu ya Dar es Salaam, alitoa maagizo kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa kufunguliwa.

“Wizara ya habari inapaswa kusimamia vyombo vya habari, nasikia kuna vijivyombo vya habari mmevifungia fungia, sijui viji- TV vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali.”

“Vifungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari, lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusu ya kuendesha chombo cha serikali anafuata sheria za serikali na kanuni ziwe wazi, kosa hili adhabu yake ni hii na mnakwenda kwa adhabu mlizoziweka kwenye kanuni, tusifungie tu kibabe. Wafungulieni lakini tuhakikishe wanafuata kanuni na miongozo ya serikali,” alisema Rais Samia

Kwenye risala ya Balile, amesema ni mara ya kwanza kwa jukwaa hilo kupata ugeni mkubwa kutoka serikalini.

“Jambo kubwa, hatujawahi kupata ugeni wa kutoka serikalini wa kufungua na kushiriki mikutano yetu tangu jukwaa hili lianzishwe mwaka 2008.

“Ni kwa mara ya kwanza leo Waziri Mkuu umekuja kuzindua mkutano wetu. Historia itakukumbuka,” amesema Balile.

Balile amesema, katika miaka minne iliyopita, vyombo vya habari nchini vimepita katika kipindi kigumu.

Kwamba, ilifika hatua kutokana na kushindwa kujiendesha, baadhi ya vyombo vikalazimika kujiondoa sokoni.

“Hali ilikuwa mbaya katika sekta ya habari kwenye kipindi cha miaka minne iliyopita.

“Baadhi ya vyombo vya habari vilishindwa kujiendesha kutokana na kutetereka kiuchumi, vikajiondoa sokoni,” amesema.

Amesema, ukiachana na sheria mbovu zilizotungwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekuwa changamoto kwa kudai kodi ya risiti za matangazo zilizotolewa na chombo cha habari hata kama hawajalipwa.

“Vyombo vinakabwa na TRA, hata kama hawajalipwa pesa za matangazo, TRA wanataka kodi, hili linakuwa gumu, tunaomba utusaidia,” amesema Balile.

Hata hivyo, Waziri Majaliwa ameagiza taasisi zote za serikali zilipe madeni ya vyombo vya habari.

Na kwamba, kama taasisi hizo hazijalipwa fedha hizo, atahitaji orodha ya taasisi hizo kwa kuwa wakati huu ni mzuri kwa kuwa ni wa bajeti ya Taifa.

Waziri Majaliwa amealikwa na jukwaa hilo kifungua mkutano. Miongoni kwa kazi zitazofanywa na jukwaa hilo ni uchaguzi wa mwenyekiti na wajimbe wa bodi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!