KATIBU Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameungana na Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), kutaka kesi zinazowakabili masheikh, katika mahakama mbalimbali nchini, ziendeshwe haraka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Sheikh Ponda ametoa wito huo jana tarehe 14 Mei 2021, kupitia waraka wake wa Idd El-Fitri, alioutoa kwa umma wa Watanzania.
Katika waraka huo, Sheikh Ponda aliishauri Serikali ipeleke ushahidi mahakamani ili masheikh hao na watuhumiwa wengine ambao kesi zao zimechukua muda mrefu, zitolewe hukumu.
“Tunaishauri serikali ipeleke ushahidi mahakamani ili mamia ya Waislamu wakiwemo masheikh, maimamu, waalimu wa madrasa, wasomi wa vyuo vikuu na waumini wa kawaida, inaowashikilia kwa tuhuma za ugaidi wapate haki yao ya kujitetea na kusomewa hukumu,” umesema waraka wa Sheikh Ponda.
Sheikh Ponda amesema “tunaikumbusha Serikali kuwa, ni kinyume na haki za binadamu kuwaweka watu gerezani na kuwatenga na shughuli zao na familia zao kwa miaka kadhaa, kwa madai ya kutafuta ushahidi.”
Wito wa Sheikh Ponda unaenda sambamba na wito uliotolewa jana na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Nuhu Jabir Mruma, katika Baraza la Iddi El-Fitri, lililofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, alikuwa mgeni rasmi.
Katika baraza hilo, Mruma aliiomba Serikali na vyombo vya utoaji haki, vishughulikie kwa haraka kesi za muda mrefu ikiwemo za Masheikh walioko mahabusu na gerezani, wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali.
Miongoni mwa Masheikh walioko mahabusu kwa tuhuma mbalimbali ni Masheikh 23 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, wanaokabiliwa na Kesi ya Jinai Na. 121/2021, katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Masheikh hao waliakamatwa mwaka 2012.
Leave a comment