August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Safari za SGR Dar – Mwanza kuanza Januari 2023

Reli ya kisasa ya SGR

Spread the love

 

TRENI ya reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es salaam kuelekea Mwanza zinatarajiwa kuanza kati ya Januari na Februari mwaka 2023. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini, Masanja Kadogosa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Shirika la Reli Tanzania TRC Jijini Dodoma.

Amesema safari hizo zitaanza mara pindi watakapokuwa wamepewa kibali na Mamlaka Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu (LATRA).

Pia amesema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kwa awamu ya kwanza Dar es salaam hadi Mwanza wenye gharama ya Sh trilioni 16 imefikia hatua nzuri na mkandarasi tayari ameshalipwa kiasi cha Sh trilioni 6.4.

Aidha, amesema kukamilika kwa reli ya kisasa kutasaidia kukuza uchumi wa Tanzania ikiwamo kukomboa muda pamoja na kufungua milango ya uchumi kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Masanja Kadogosa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC)

Pia amewatoa hofu Watanzania kuhusu kukatika kwa umeme katika usafiri wa reli ya kisasa na kubainisha kuwa treni zitakazotumia reli hiyo zinaweza kufua umeme wake na kusafiri zaidi ya dakika 48 bila umeme wa gridi ya Taifa.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo kwa mwaka 2021/2022-2022/23 umejikita zaidi katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa shirika kwa kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya reli.

Aidha, ameeleza ili kufikia lengo la Shirika ni kuboresha miundombinu ya reli kwa kujenga mtandao mpya wa reli ya kiwango cha SGR wenye jumla kilometa 4777 na kukarabati mtandao wa reli iliyopo ya Meter Gauge kwa kilometa 2,537.

error: Content is protected !!