January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Safari ya mwisho ya Komba

Wananchi waliojitokeza kumuaga Kapteni John Komba

Spread the love

MAJONZI, vilio na simanzi vimetawala kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba. Anaandika Pendo Omary…(endelea).

Rais Jakaya Kikwete, ndiye aliwaongoza maelfu ya waombolezaji katika viwanja vya Karimjee.

Shuhuli hiyo, ilianza saa tano asubuhi na kuhitimishwa saa nane mchana ambapo salaamu mbalimbali za rambirambi zilitolewa kutoka kwa viongozi wa serikali, vyama huku makundi ya sanaa aliyoitumikia Komba, vikiwasilisha salamu zao kwa nyimbo.

Kiongozi wa upinzani

Salamu za Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema) ndizo zilisomwa za kwanza kupitia kwa mwakilishi wake Joshua Nasari- Mbunge wa Arumeru Mashariki.

“Tulikuwa tofauti katika itakadi za kisiasa, lakini marehemu Komba ni binadamu wenzetu, hivyo ni lazima tuweke itakadi zetu pembeni.

“Wakati wote tunapaswa kutenda mema kwa familia na taifa kwa sababu hatuna muda wa kudumu hapa duniani,” amesema Nasari

Kauli ya CCM

Kwa niamba ya Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana amesema, kifo cha Komba kimeacha pengo ndani ya CCM, familia ya marehemu na watanzania. Hivyo, watanzania wanapaswa kumuenzi kwa kuzingatia mema yake.

“Komba alikuwa ndugu; rafiki; alipedwa na wengi; alikuwa na vipaji vingi ikiwemo msanii, mwanajeshi, mbunge mahili, mzalendo kwa nchi yake, mwaminifu kwa chama chake na kwa wananchi aliowaongoza.

“Pia alikuwa na kipaji cha kutunga nyimbo zilizoendana na wakati na mazingira. Tunatoa rambirambi yetu ya shilingi milioni tano kama mchango kwenye msiba huu,” amesema Kinana.

Serikali

Mwakilishi wa Serikali, Jenusta Mhagama-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), amesema, kifo cha Komba kimewagusa watu wengi.

Anasema kuwa anakumbukwa kwa kuwaunganisha watanzania wakati wa msimba wa hayati Baba wa taifa, mwalimu Julius Nyerere hasa kwa nyimbo zake.

“Alituunganisha wakati wa msiba wa Baba wa Taifa. Serikali inawahakikishia wananchi wa jimbo la Mbiga Magharibi kuwa, itaendeleza mipango aliyoiacha marehemu Komba ya kuwaletea maendeleo kwa kuzingatia ilani ya CCM na mipango ya serikali,” amesema Mhagama.

Baraza la Wawakilishi

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Abdalla Ally Abdalla amesema “marehemu alikuwa mchangiaji mzuri katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Zanzibar tumepata pengo kubwa. Tunachangia shilingi milioni moja katika kuifariji familia ya marehemu,” amesema.

Bunge la Jamhuri

Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema Komba ameondoka kama moto wa kibatari uliozimika ghafla. Hali iliyompta Komba ingeweza kumapta mtu yoyote.

Aidha, Makinda amewataka Watanzania kuacha kumtukana marehemu katika mitandao ya kijamii kwa kuwa sasa hawezi kujitetea.

“Mungu angempa Komba dakika 15 za kujitetea kabla ya umauti kumkuta, hakika angewaomba msamaha wale wote waliomkosea. Hivyo na sisi tunapaswa kumsamehe. Pia ni muhimu kuwa makini kwa yale tunayoyanzungumza, kwa kuwa mdomo huumba,” amesema Makinda.

Familia

Akizungumza kwa niaba ya familia, Dominic Mwakangale amesema “hatukutarajia kupata msiba huu katika muda huu. Tunatoa shukrani za dhati kwa watanzania wote kwa kutufariji katika msiba huu hasa serikali, CCM na Bunge. Mmetutia nguvu. Tumefarijika”.

Komba alizaliwa 18 Machi, 1954 katika kijiji cha Lituhi Nyasa, Ruvuma. Alifariki 27 Machi mwaka huu baada ya kuugua ghafla na kukimbizwa katika hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.

Mwili wa marehemu Komba utazikwa Jumanne hii nyumbani kwake katika kijiji cha Lituhi Nyasa, Ruvuma.

 

error: Content is protected !!