Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Safari ya mabadiliko yaweza kufia njiani  
Habari za SiasaTangulizi

Safari ya mabadiliko yaweza kufia njiani  

Edward Lowassa, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema (wakwanza)akiteta jambo na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF
Spread the love

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Dimani, Unguja na kwenye kata 20 Tanzania Bara, yametushutua wengi. Miongoni mwa yayosababisha mshutuko, ni kushindwa vibaya kwa wagombea wa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo, anaandika Mwandishi Wetu.

Ni kwa sababu, kwa muda mrefu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa kikionekana machoni mwa wengi kinatawala bila kufikiri matokeo yake kwenye sanduku la kura.

Katika uchaguzi huo, CCM kimepata ushindi kwenye kata 19, kati ya 20 zilizofanya uchaguzi na kimeibuka mshindi pia katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Dimani.

Huu ni uchaguzi wa kwanza kufanyika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Ulikuwa ni uchaguzi kati ya wenye mawazo mapya yenye maono na mifumo tofauti na wale kutoka kwenye mfumo wa kale wa nusu karne.

Kama zilivyo chaguzi nyingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza kuwa uchaguzi huo, “ulikuwa huru na haki na uliendeshwa kwa misingi ya sheria, katiba na kanuni.”

Hata hivyo, siyo kweli kwamba uwanja wa uchaguzi ulikuwa huru na haki. Wala siyo kweli kuwa uchaguzi huu uliendeshwa kwa uwazi na kusimamiwa na watu wenye weledi.

Wala haiwezi kuwa kweli kwamba uchaguzi huo uliendeshwa kwa kufuata sura ya 343 ya sheria inayounda NEC na; au sura ya 292 ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika baadhi ya maeneo, hasa jimboni Dimani, upo ushahidi kuwa kilichofanyika sicho kinachoelezwa na NEC. Dimani hakukuwa na uchaguzi. Kulikuwa na hujuma dhidi ya matakwa ya wananchi. 

Yapo madai yanayoweza kuthibitishwa, kuwa baadhi ya mawakala wa wagombea ubunge katika jimbo hilo wanaotokana na vyama vya upinzani, walitolewa nje ya vituo vya kupigia na kuhesabu kura.

Miongoni mwa mawakala walioripotiwa kutolewa nje ya vituo, ni pamoja na Abeid Majid Abeid na Yunus Masoud Gharib, waliokuwa kwenye kituo cha Bweleo na Abdi Mustafa Habib, aliyekuwa katika kituo cha Uwandani.

Abeid anadai alikuwa chumba Na. 1 na Gharib alikuwa chumba Na 2, huku Habib akiwa chumba namba sita. Wote walikuwa mawakala wa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdulrazak Khatib Ramadhan.

Abdulrazak alilalamikia kitendo hicho kwa mkurugenzi wa NEC, jijini Dar es Salaam, kabla ya matokeo kutangazwa na zoezi la upigaji kura kumalizika. Lakini hakuna aliyemsikiliza.

Wengine wanaodaiwa kutolewa nje ya vituo, ni Shani Khatib Khamis, Mbarouk Ali Haji, Suleiman Othman Omar na Ibrahim Muharam Mwinyi, ambao walikuwa mawakala wa chama cha National Reconstruction Allience (NRA) na CHAUMMA. 

Katika barua yake kwenda kwa mkurugenzi wa NEC, Abdulrazaki anasema, “uchaguzi wote ulisimamiwa na vyombo vya dola na uliendeshwa moja kwa moja na jeshi la wananchi na jeshi la polisi.”

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyobeba Kumb. REF/AB/T/001/2017, Abdulrazaki anasema,

“kazi ya kuwatoa nje mawakala wa upinzani ilifanywa na polisi” na kuongeza, “uchaguzi unaoendeshwa kwa mtindo huu, hauwezi kuitwa uchaguzi wa haki na huru na hauwezi kuakisi maamuzi ya wapiga kura.”

Katika baadhi ya maeneo, kuliibuka malalamiko kuwa wapiga kura halali kuondolewa kwenye vyumba vya kupigia kura na kuingizwa wapiga kura wasiostahili, wakiwamo kutoka nje ya kata (shehia) za jimbo hilo.

Baadhi ya wapigakura “mamluki” walitumia shahada za watu waliofariki dunia. Miongoni mwa wanaotajwa kuwa shahada yake ilitumika wakati mwenyewe akiwa tayari amefariki, ni Samia Khatib Ramadhan, ambaye alikuwa dada wa mgombea wa CUF.

Samia amefariki dunia tarehe 5 Januari mwaka huu. Lakini amenakiriwa katika walioshiriki uchaguzi wa 22 Januari 2017 katika kituo kilichokuwapo shule ya Dimani.

Yamekuwapo hata madai kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK), lililotumika kwenye uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 kwenye jimbo hilo, siyo lililotumika kwenye uchaguzi wa Jumapili iliyopita. Huko ni Unguja.

Lakini kwa upande wa Tanzania Bara, kilichosababisha CCM kuibuka na ushindi mnono katika uchaguzi huu, kumesababishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutowekeza kwenye chaguzi hizo za kata.

Badala yake, tumekishuhudia chama hicho kikitumia nguvu kubwa na rasimali nyingi, kuwekeza kwenye chaguzi za kanda.

Karibu viongozi wake wote wakuu, akiwamo mwenyekiti wa taifa, Freeman Mbowe, katibu mkuu, Dk. Vicenti Mashinji; wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Prof. Mwesiga Baregu na baadhi ya wabunge, waliweka kambi eneo la Ziwa Victoria, kwenye chaguzi za ndani ya chama.

Makosa haya ndiyo yaliyofanyika kwenye uchaguzi mkuu uliyopita. Chama hiki kiliweka nguvu kubwa kwa mgombea wake wa urais, badala ya kuwekeza kwa wagombea wake wa ubunge.

Hakuna kokote ambako chama hiki kiliwahi kufanya uchambuzi yakinifu wa kubaini nguvu na ushawishi wa Lowassa kwenye uchaguzi ule. Lowassa alikuwa na mpaka sasa, amebaki kuwa mwanasiasa pekee nchini mwenye ushawishi mkubwa kwa wapigakura.

Hivyo basi, kama Chadema kingefanya tathimini na kingekuwa na mipango thabiti, kingebaini kuwa nguvu zilizotumika kumnadi Lowassa, hazikuhitajika, badala yake nguvu hizo zingeelekezwa kwenye majimbo. Lowassa alikuwa na nguvu zake binafsi na alikuwa anauzika.

Hilo lingefanyika, madai kuwa kura zimeibwa yasingekuwapo. Kilichopatikana kwenye sanduku la kura ndiko kingetangazwa.

Hata kama Lowassa angeshindwa kwenye uchaguzi ule, bado upinzani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ungeshinda majimbo mengi kuliko CCM. Ushindi huo ungetoa fursa kwa mara ya kwanza, waziri mkuu kutoka upinzani na hivyo upinzani kuwa sehemu ya serikali.

Lakini kutokuweza kwenye majimbo kumesababisha zaidi ya majimbo 40 kushindwa kwa kupata kura kati ya asilimia 46 na 49.

Makosa hayohayo yameendelezwa kwenye uchaguzi huu.

Ukiondoa Dimani ambako CUF, kiliwekeza vema, kwenye kata karibu zote uwekezaji ulikuwa ni mdogo na; au haukuwapo kabisa.

Ni sawa na kutaka mavuno, lakini papo hapo hutaki kulima au kulinda wanyama wanaoharibu mazao.

Hata dakika za mwisho za uchaguzi bado Chadema waliendelea kujiamini kuwa kitashinda uchaguzi huo.

Kwa muda mrefu hasa katika miaka hii mitano iliyopita, wanachama wa chama hiki kutoka ndani na wakosoaji kama mimi (kutoka nje) ambao bado tumekuwa na mapenzi na Chadema, tumejaribu kukikosoa ili kitumie muda huo kujisahihisha.

Matokeo haya ni mabaya kuliko yote ambayo upinzani umeyapata tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini, kuanzia Kwahani, (Unguja), Ileje (Mbeya), Morogoro Kaskazini, Magu (Mwanza), ambako mgombea wa upinzani, John Cheyo alifanikiwa kuibwaga CCM.

Baadaye upinzani ukainyang’anya CCM jimbo la Temeke.

Hata Kiteto, Busanda, Tunduru, Biharamulo, Igunga na Uzini (Unguja), upinzani ulifanya vizuri na imekuwa ikipanda kulinganisha na uchaguzi huu. Upinzani ulifanikiwa kurejesha jimbo la Tarime (Chadema) na kuinyang’anya CCM jimbo la Arumeru Mashariki (2012).
Kwa upande wa madiwani ni hivyo hivyo. Haijawahi kutokea katika uchaguzi wa marudio, upinzani ukashindwa kulinda au kuongeza idadi ya kata zake. Chaguzi za marudio zilitumika kuweka msingi wa kushida majimbo hayo; ndivyo ilivyokuwa Kigoma Mjini, Biharamulo na kwingineko.

Kwa mtu yeyote aliyefuatilia siasa nchini aliona mapema dalili za Chadema kunyeshewa mvua kwenye uchaguzi huu. Ni baada ya kushindwa kuchukua hatua za ziada hasa katika kumpata mrithi wa Dk. Willibroad Slaa, aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Ninaamini kabisa kuwa kama Chadema kingeweka nguvu japo kidogo tu, matokeo ya uchaguzi huu yasingekuwa kama yalivyo sasa.

Wapigakura wa Tanzania wasije kudharauliwa tena na mtu yeyote kuwa hawajui kuchagua au hawaoni. Wapigakura nao kama binadamu wana kikomo chake.

Kitendo cha kutowekeza kwenye uchaguzi huo, kumesababisha Chadema kuwa ya mwisho katika baadhi ya maeneo.

Kwa mfano, katika kata ya Nkome, wilayani Geita, Chadema kilishika nafasi ya nne, nyuma ya ACT-Wazalendo. Nafasi ya pili ilichukuliwa na CUF.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, CCM kilipata kura 2922, CUF kura 1972, ATC-Wazalendo kura 536 na Chadema kiliambulia kura 167.

Kuanguka kwa Chadema katika uchaguzi huu, kumesababishwa kwa kiwango kikubwa na hatua ya Ibrahim Lipumba, kuamua kuvuruga upinzani kwa makusudi.

Lipumba ndiye aliyekuwa mwasisi wa UKAWA wakati wa Bunge Maalum la Katiba na sasa ndiye anayetenda dhambi ya kuungamiza.

Alizunguuka ulimwenguni kote na kuhubiri kuwa “vyama vya upinzani vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwa kila nafasi, kuanzia serikali za mitaa, ubunge, uwakilishi na urais.”

Mradi wa Prof. Lipumba wa kusimamia wagombea kinyume na mapatano ya UKAWA, ulilenga kupunguza nguvu ya upinzani kushinda. Katika hili amefanikiwa.

Kwa kauli yake mwenyewe, Prof. Lipumba alisema, “kauli mbiu yetu katika kampeni itakuwa paza sauti, pinga ufisadi wa Chama Cha Mapinduzi na Chadema.”

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!