RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, ameitaka mamlaka ya Serikali Wilaya ya Chato mkoa wa Geita, kukamilisha haraka mchakato wa kuifanya Chato kuwa mkoa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, katika salamu zake kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Dk. Magufuli alifariki dunia Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na unazikwa leo Ijumaa 26 Machi 2021, nyumbani kwao Chato mkoani Geita.
Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Mgufuli akizindua Hospital ya Rufaa ya Chato
“Nina taarifa mchakato umeanza na ninaagiza mamlaka za chini, mkimaliza mchakato huku mtuletee tuangalie kama vigezo vimekidhi, kuwa mkoa siyo tatizo na kama vigezo havikukidhi, tutawaelekeza.”
“Na ili kumuenzi mpendwa wetu, kamilisheni tuone jinsi ya kufanya,” amesema Rais Samia
Kauli hiyo, ilikuwa anajibu maombi ya wazee wa Chato waliyoyatoa awali, kuwa enzi za uhai wake, Dk. Magufuli ambaye ni mzaliwa wa Chato, aliahidi kuifanya Chato kuwa mkoa.
Ombi hilo lilitolewa na Mzee Charles Bigambo alipokuwa akitoa salamu za wazee wa Chato.
Aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Magufuli akiwa kwenye Uwanja wa ndege wa Chato enzi za uhai wake
Katika salamu zake fupi, kwenye Uwanja wa Mpira wa Magufuli akisema “leo niko Chato kwa mara ya tatu, mara ya kwanza nilikuwa Chato kwenye kampeni za mwaka 2015.”
“Mara ya pili nilikuja kumfariji kaka yetu, Dk. Magufuli kwa kuondokewa na dada yake (Minica Joseph Magufuli, mwaka 2018), na sasa nimerudi Chato, kwa dhumuni la kumuhitimisha kiongozi wetu, kaka yetu, baba yetu, mlezi wetu, mwalimu wetu kuja kumweka kwenye nyumba yake ya milele,” amesema Rais Samia
“Nilipokuja kumpa faraja, alinionyesha eneo ambalo ndugu zake wanakuwa wanasitiliwa, sikujua kama nitakuja Chato kumstili eneo ambalo alikuwa ananionyesha. Ni mambo mazito na msiba huu ni wetu sote na familia hatutawaacha,” amesema
Uwanja wa Ndege wa Chato wakati unajengwa
Rais Samia amesema “Wanachato, mpendwa wenu ameondoka, mnajiuliza itakuwaje, nataka kuwahakikishia ni kutekeleza miradi yote iliyomo kwenye ilani ya uchaguzi na zile alizotoa yeye mwenyewe na si kwa wana Chato bali ni nchi nzima.”
Leave a comment