May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sabaya asomewa shtaka la kumpora diwani CCM Sh. 390,000

Lengai ole Sabaya

Spread the love

 

LENGAI Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro na wenzake wawili, wamesomewa mashtaka mawili ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, wanaodaiwa kumfanyia Diwani wa Sombetini (CCM), Bakari Msangi na kumuibia Sh. 390,000. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).

Mashtaka hayo mawili waliyosomewa, ni kati ya sita yanayowakabili pamoja na washtakiwa wengine watatu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Sabaya na wenzake, Sylvester Nyingu ‘Kicheche’ (26) na Daniel Mbura (38), walisomewa mashtaka hayo leo Ijumaa, tarehe 18 Juni 2021 na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tarsila Gervas, katika mahakama hiyo.

Akiwasomea shtaka hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha, Gervas amedai kuwa, washtakiwa hao walilitenda tarehe 9 Februari 2021, kwenye Mtaa wa Bondeni, jijini Arusha, ambapo walivamia duka linalomilikiwa na Said Saad, kisha kuwaweka chini ya ulinzi baadhi ya watu waliokuwepo katika eneo hilo.

Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, akiwasili mahakamani

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa, katika tukio hilo Sabaya na walinzi wake walimfunga pingu Msangi na kumuibia kiasi cha Sh. 390,000.

Sabaya na wenzake wanaotetewa na Wakili Moses Mahuna, wanadaiwa pia kumpiga mateke na kumtishia silaha, Ramadhani Ayoub, kisha kumpora simu na Sh. 35,000. Hata hivyo, Sabaya na wenzake walikana mashtaka hayo.

Sabaya na wenzake walisomewa mashtaka hayo, Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha, baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka, kudai kwamba upelelezi wa mashtaka hayo, umekamilika.

Baada ya washtakiwa hao kuyakana makosa hayo, Hakimu Mshasha aliiahirisha kesi hiyo, hadi tarehe 2 Julai 2021.

 

Sabaya na wenzake wamerudishwa tena rumande katika Gereza Kuu la Kisongo, jijini humo.

Mwanasiasa huyo alianza kukumbwa na misukosuko baada ya kuondolewa madarakani na Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 13 Mei 2021, ambapo kiongozi huyo aliagiza achunguzwe kufuatia tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka mengine manne, ambayo upelelezi wake unadaiwa bado haujakamilika, ikiwemo uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, kuunda genge la uhalifu na kuomba rushwa. Baadhi ya mashtaka hayo hayana dhamana.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo tarehe 4 Juni 2021, baada ya kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa siku kadhaa.

error: Content is protected !!