ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya amebubujikwa machozi mahakamani wakati akimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kutizama kesi zinazoendelea dhidi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Sabaya amefikisha kilio hicho kwa mkuu wa nchi leo Jumatano, tarehe 01 Juni 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro aliposomewa mashtaka saba pamoja na wenzake yakiwemo ya kuendesha genge la uhalifu na utakatishaji fedha.
Mashtaka mengine ni rushwa na matumizi mabaya ya madaraka akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Mbali ya Sabaya wengine kwenye kesi hiyo ni Silivester Nyegu, John Aweeyo, Nathan Msuya na Antero Assey ambapo wamesomewa mashtaka na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka
Kabla ya kesi hiyo kuahirishwa hadi tarehe 7 Juni 2022 kwa watuhumiwa kurejeshwa Gereza Kuu la Karanga Mkoa wa Kilimanjaro, Sabaya alinyoosha mkono na kusimama na kuanza kumshushia tuhuma nzito mwendesha mashitaka Mkuu wa serikali, Tumaini Kweka akidai mashitaka yanayoendelea ni ya kisiasa yenye lengo la kumuumiza kisiasa.
“Mheshimwia hakimu, hatuna imani na incharge wa kesi hii, Kweka anatokea Wilaya ya Hai ambako mimi nilikuwa mku uwa wilaya, kazi anayoifanya Kweka ni kumuumiza Sabaya,” amedai
Huku akibubujikwa na machozi, Sabaya amesema ni vizuri Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akajua kuwa wanachofanyiwa ni uonevu na kuzitaka mamlaka kuwatendea haki huku akidai wana imani na ofisi ya mwendesha mashitaka lakini si Kweka.
Leave a comment