HAKIMU Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Wilbard Mashauri, ametoa sababu kubwa tano alizofikia kufanya maamuzi ya kufuta dhamana za viongozi wawili wandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Washitakiwa waliofutiwa dhamana, ni mwenyekiti wa chama hicho taifa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe na mbunge wa chama hicho katika jimbo la Tarime Mjini, Ester Matiko.
Akisoma uamuzi wake huo jana Ijumaa, tarehe 23 Novemba, Hakimu Mashauri alitaja sababu hizo kama ifuatavyo:
Kwanza, Hakimu alisema, washitakiwa wote wawili – Mbowe na Matiko – wamethibitika kuidharau mahakama na kukiuka masharti ya dhamana waliyopewa katika kesi ya msingi iliyokuwa inawakabili mahakamani hapo.
Akichambua hoja kwa mshitakiwa mmoja juu ya mwingine, Hakimu Mashauri alisema, mshitakiwa Na. 1 – Freeman Aikael Mbowe – ameshindwa kuithibitishia mahakama pasipo na shaka kuwa alikuwa mgongwa na alishindwa kurejea nchini kuendelea na kesi yake kwa sababu ya ugonjwa huo.
Alisema, Mbowe alieleza mahakama kuwa aliondoka nchini, tarehe 28 Oktoba 2018, kwenda Washington DC, nchini Marekani, kuhudhuria mkutano wa tarehe 30 na 31 Oktoba.
Alisema, alidai kuwa usiku ya siku ambayo alitakiwa kurejea nchini ili aweze kuhudhuria kesi yake mahakamani, ghafla aliugua.
Hakimu Mashauri alisema, “Mbowe ameshindwa kufika mahakamani terehe 1 Novemba na 8 Novemba, huku akijua kuwa kufanya hivyo ni makosa.
Pili, Hakimu Mashauri alisema, mshitakiwa huyo alieleza mahakama kuwa alishindwa kurejea nchini kutokana na kupata maradhi na kushauriwa na madaktari wake asisafiri umbali mrefu kwa ndege.
“Lakini hati yake ya kusafiria, inaonyesha kuwa alisafiri umbali mwingine mrefu kwa usafiri huo huo wa ndege, jambo linalothibitisha kuwa alikuwa akiiongopea mahakama na kuidharau kwa makusudi.”
Alisema, “huu ni uongo, kwa sababu, katika hati yake ya kusafiria, inaonekana alisafiri kutoka Marekani kwenda Brussels, nchini Ubelgiji, tarehe 2 Novemba huku akitakiwa mahakamani 1 Novemba.
“Haiwezi kuingia akilini, kwamba daktari amemzuia mshtakiwa kusafiri kwa ndege kutokana na ugonjwa wake, huku mgonjwa huyo huyo, akitumia usafiri wa ndege kwenda nchini Ubelgiji. Haiwezekaani.”
Tatu, Mashauri alisema, Mbowe kwa mujibu wa hati yake ya kusafiria iliyopo mahakamani, amekaa Ubelgiji kuanzia terehe 1 Novemba hadi 6 na kusafiri tena kwenda Dubai kwa ajili ya matibabu.
Hakimu Mashauri anasema, “mshitakiwa ameeleza mahakama kuwa alitakiwa kupumzika. Lakini nyaraka zake za matibabu zinaonyesha terehe 8 Novemba, alipata matibabu Dubai kwenye nchi za Falme za Kiarabu (UAE), wakati akijua alitakiwa kuwapo mahakamani.
Nne, Hakimu Mashauri alisema, “hata mdhamini wake, aliiongopea mahakama kuwa Mbowe alienda Afrika Kusini akiwa mahututi na hakuweza kuongea. Lakini mshitakiwa mwenyewe ameeleza kitu tofauti mahakamani.”
Tano, washtakiwa hao wawili, wameshindwa kufika mahakamani tarehe 1 na 8 Novemba mwaka huu bila kutoa sababu za msingi.
Alisisitiza, “Mbowe alikuja mahakamani kuzungumza mambo ya uongo.”
Akizungumzia kuhusu Matiko, Hakimu Mashauri alisema, nchi inaongozwa na sheria na ni matakwa kwamba mshtakiwa akikabiliwa na makosa ya jinai pamoja na vyeo vyao bado wanatakiwa kuwepo mahakamani.
“Maelezo aliyoyatoa Matiko kwanini asifutiwe dhamana hayakidhi matakwa ya yeye kushindwa kuhudhuria mahakamani wakati kesi ilipokua inakuja kwa ajili ya kutajwa. Huyu alikuwa analeta dharau kwa mahakama,” alisisitiza.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mashauri alisema, mahakama imeamua kuwafutia dhamana zao Mbowe na Matiko na kurudishwa mahabusu mpaka shauri lao litakapomalizika.
Alisema, sababu alizozitoa mshitakiwa huyo kuwa alihudhuria ziara ya kibunge nchini Burundi, hazikidhi matakwa ya kutofika kwake mahakamani.
Kwenye kesi hiyo Na. 112 ya mwaka 2018, Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro, ni mshtakiwa wa Na 1 na Matiko ni mshitakiwa namba tano.
Mbowe, anakabiliwa na mashitaka saba, yakiwamo kuhamasisha vurugu, kufanya maandamano bila kibali, kuhamasisha maasi na kusababisha mauaji ya mwanafunzi wa chuo cha taifa cha usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.
Naye Matiko, anakabiliwa na mashitaka matatu, likiwamo la uchochezi na kuhamasisha maandamano. Washitakiwa hao wawili, pamoja na wengine saba, walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza 27 Machi mwaka huu.
Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo, ni pamoja na katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji; manaibu katibu mkuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.
Wengine ni Halima James Mdee, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA) na mbunge wa Kawe; mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Katika kesi hiyo, upande wa utetezi unaoongozwa na wakili wa kujitegemea, Peter Kibatala, umeeleza mahakama kuwa inapinga maamuzi hayo na hivyo, wanakusudia kufungua kesi mahakama kuu.
Alisema, maamuzi yao ya kukata rufaa yamejiegemeza kwenye chini ya kifungu cha 161 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 20 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kifungu hicho kinaeleza kuwa amri zote za dhamana zinaweza kukatiwa rufaa au kufanyiwa marejeo na Mahakama Kuu.
Upande wa mashitaka unaongozwa na mawakili, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Simon Wankyo na Dk. Zainab Mango, uliiambia mahakama kuwa haina pingamizi na uamuzi huo.
Hata hivyo, mawakili wa serikali waliiomba mahakama hiyo kuendelea na hatua ya usikilizwaji na kwamba wana mashahidi wapo tayari kuendelea.
Hoja hiyo ilipingwa na Kibatala ambaye aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo kwa sababu hawako tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi na kwamba mahakama ijielekeze kuwapatia nakala ya uamuzi.
Alidai washtakiwa wana haki ya kupeleka rufaa mahakama kuu hivyo wanataka mchakato uanze mara moja.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Nchimbi alidai hoja za ahirisho zinakosa sapoti za sheria na taratibu kwani mara ya mwisho shauri hilo lilipokuwa linaahirishwa, mahakama ilisema inaahirishwa kwa ajili ya uamuzi na kuendelea na usikilizwaji.
Alidai masuala yanayohusiana na dhamana ni tofauti na kusikilizwa kwa kes hiyo, hivyo mahakama itupilie mbali maombi hayo na iruhusu kuendelea kusikilizwa.
Mara baada ya mabishano hayo ya kisheria, Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi saa 7:30 mchana jana, ili aweze kutoa uamuzi wa kuendelea na kesi hiyo au la.
Wakati kesi hiyo ilipoahirishwa, Wakili Kibatala, alifungua maombi ya dhamana Mahakama Kuu ambayo yanasubiri kupangiwa tarehe ya kuanza kutajwa.
Ilipofika saa 7:30, Hakimu Mashauri alisema, upande wa washtakiwa umefungua rufaa ya maombi ya dhamana kwa wateja wao kwa sababu ni haki yao ya msingi.
Alisema wakati rufaa hiyo ikiendelea katika Mahakama Kuu, washtakiwa hao wataendelea kukaa mahabusu mpaka uamuzi utakapotolewa.
Alisema, “baada ya upande wa washtakiwa kufungua kesi ya rufaa ya kupinga uamuzi wa kuwafutia dhamana, washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu mpaka uamuzi utakapotolewa na Mahakama Kuu.”
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo mpaka tarehe 6 Desemba kwa ajili ya kutajwa huku Mbowe na Matiko wakitarajiwa kutokea mahabusu.
Leave a comment