October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sababu ya kifo cha Benjamin Mkapa yatajwa

Hayati Benjamin Mkapa

Spread the love

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita, jijini Dar es Salaam, amefikwa na mauti, kwa mshutuko wa moyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza mbele ya maelfu ya waombolezaji waliofurika kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Willium Urio, ambaye ni msemaji wa familia ya rais mstafu Mkapa amesema, mwanasiasa huyo amekutwa na mauti kwa mshutuko wa moyo na akiwa amekaa.

Urio alitoa kauli hiyo, wakati wa Misa ya kuaga mwili wa kiongozi huyo, ambaye alikuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1995 na 2005.

Akieleza hatua kwa hatua safari ya mwisho ya Mkapa kuanzia kuumwa kwake hadi kifo chake, Urio alisema, “napenda kutumia fursa hii, kueleza umma, kwamba mzee wetu (Benjamin Mkapa), alikuwa hajisikii vizuri. Akaamua kwenda hospitali, (kwenye vipimo) na huko alionekana kwamba alikuwa na ugonjwa wa malaria.

         Soma zaidi:-

Alisema, Mkapa alianza kupata matibabu na kisha kulazwa siku ile ya Jumatano, na siku iliyofuata ambayo ni Alhamisi mchana, aliendelea vizuri.

Alisema, wakati huo, Mkapa alikuwa anaangalia maonesho yaliyokuwa yakioneshwa mubashara ya chaguzi zilizokuwa zikiendelea kwa wanaogombea ubunge wanawake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Urio amesema, “baada ya hapo, alisikiliza taarifa ya habari. Nami nikaagana naye pamoja na wanafamilia wengine. Baadaye tukaondoka.”

“…baada ya kusikiliza taarifa ya habari alitaka kuinuka kutaka kutoka. Alipoinuka, akakaa na akainamisha kichwa na hivyo, mpaka walipokuja kumpima, akathibitika kwamba amefariki dunia. Sababu yake ya kifo alipata mshtuko wa moyo.

Rais mstaafu Benjamin William Mkapa, aliingia madarakani Novemba mwaka 1995, kuchukua nafasi ya Rais Alli Hassan Mwinyi, ambaye alichukua madaraka ya urais, kutoka kwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mwili wa kiongozi huyo, umeanza kuagwa leo Jumapili tarehe 26 hadi Jumanne tarehe 28 Julai 2020, katika uwanja wa michezo wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Mazishi ya Mkapa aliyezolea sifa katika kufufua na kusimamia uchumi, yatafanyika kijijini kwake, Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara, siku ya Jumatano tarehe 29 Julai mwaka huu.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari mbalimbali

error: Content is protected !!