January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sababu 40 za kuipinga Katiba inayopendekezwa

Katiba Inayopendekezwa

Spread the love

ZIPO sababu zaidi ya 100 za kuikataa katiba inayopendekezwa, kwa leo tutaangazia sababu 40 za kupinga katiba hiyo. Sababu hizo zimegawanyika katika sehemu mbili kimchakato na kimaudhui.

Sababu ya kwanza ni kupuuzwa kwa maoni ya wananchi kama ilivyoainishwa katika rasimu ya pili ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyozunguka nchi nzima ikakusanya maoni.

Pili ni matatizo ya kimchakato yalianzia kwenye muundo wa Bunge Maalumu lililoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Bunge hili lilijaa wanasiasa kwani lilikua lina wabunge wote, wawakilishi wote hivyo kufanya idadi ya wanasiasa kuwa robo tatu ya Bunge lote. Hata wajumbe 201 ndani yake kulikua na wanasiasa 40 wawakilishi wa vyama.

Vile vile kulikuwa na wawakilishi wa AZAKI ambao ni makada wakongwe wa vyama vya siasa suala lililosababisha majadiliano kuelekea mrengo wa kisiasa.

Bunge la Katiba lilikosa uhalali wa kisheria na kisiasa pale lilipoendelea na majadiliano ilhali baadhi ya wajumbe walikua wametoka nje ya ukumbi, ingepaswa maridhiano yafanyike ndipo Bunge hilo liendelee.

Katika suala la upigaji kura, kuliwekwa kwa makusudi kura za wazi na za siri ili kuwabana wanachama ambao watakwenda kinyume na maslahi ya vyama husika.

Kuwekwa kwa kanuni ya kuruhusu upigaji kura kwa watu waliyoko Hospitali India, Hija na kwingineko ilimradi akidi itimie.

Licha ya kufanya hivyo, bado akidi hazikutimia kwa kuwa wabunge wengi wa Zanzibar walitoka na Ukawa, hivyo hata akidi za kamati mbalimbali walipokua wanajadili rasimu ya Katiba hazikutimia.

Kuwepo kwa kura za watu wasiokuwepo na waliokufa; kwa mfano mjumbe Shida Salum wa kundi la 201 alihesabiwa kuwa amepiga kura. Vile vile mjumbekutoka Zanzibar, ambaye pia ni Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Khamis Ambari Haji alihesabika kuwa amepiga kura wakati hakuwepo bungeni.

Sababu nyingine ya kupinga katiba iliyopendekezwa ni kuondoa nguvu ya wananchi wapiga kura kuwawajibisha wabunge wao ambao hawawajibiki majimboni kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya pili Ibara ya 129. Kifungu hiki cha uwajibikaji kimeondolewa hakipo kwenye katiba inayopendekezwa.

Kuwepo kwa vifungu vya “urembo” kwa mfano haki ya afya na maji safi ambazo utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa rasilima kama ilivyoainishwa ktaika Ibara ya 129 kifungu cha 4 cha katiba inayopendekezwa, huku ni kukosekana kwa umakini wa serikali.

Katiba inayopendekezwa ina mkanganyiko kwa sababu imechanganya haki za makundi ambayo mahitaji yao yanafanana; mfano haki za wakulima na wafugaji, wavuvi na wachimba madini-Ibara ya 46 ya katiba inayopendekezwa.

Mambo haya yanaingizwa pasipo kutilia maanani tofauti ya wachimbaji wadogo na wakubwa, wakulima wadogo na wakubwa na hata wavuvi wadogo.

Kuondolewa kwa Tunu za uwajibikaji, uwazi na uadilifu iliyoko kwenye Ibara ya 5 rasimu ya pili, ni ngumu kuwa na taifa imara, uongozi bora bila uwajibikaji, uwazi na uadilifu.

Katiba inayopendekezwa imeondoa ukomo wa wabunge, katika rasimu ya pili iliweka kikomo cha mihula miwili tu katika Ibara ya 125 kifungu cha (2)(a). Katiba hiyo ikipita italeta uongozi wa kifalme usiokuwa na kikomo, mbunge ataweza kukaa maisha yake yote.

Suala lingine ni kuongezeka kwa madaraka ya Rais kuliko hata ilivyokua kwenye Katiba ya mwaka 1977, ibara za 80 mpaka 86 na ibara za 93 mpaka 98. Suala la ambalo ni hatari iwapo atatokea rais ambaye si mwaminifu na mwadilifu anaweza kutumia madaraka yake vibaya na kuipeleka nchi pabaya.

Haki ya kuishi sio thabiti kwani iko kwa mujibu wa sheria. Hii inalea kuendelea kuwepo kwa adhabu ya kifo kama inavyoeleza ibara ya 33 ya katiba inayopendekezwa.

Katiba inayopendekezwa inaeleza sifa za mbunge ajue kusoma na kuandika tu, Ibara ya 140 (a). Watunzi wa Katiba hawataki watu watakaoweza kuchambua mambo bungeni na kuihoji serikali.

Haya ni baadhi ya mambo yanayofanya katiba iliyopendekezwa kuonekana kuwa sio ya wananchi bali ni ya watawala. Katika makala ijayo tutaendelea na sabubu nyingine za kuipinga Katiba inayopendekezwa.

Mwandishi wa makala haya ni Ferdinand Shayo, Arusha, anapatikana kwa ferdinandshayo@gmail.com, 0765938008

error: Content is protected !!