April 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Saba mbaroni wakihusishwa vifo vya watu watano Ukerewe

Spread the love

WATU saba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya watu watano akiwemo Ibrahim Njalali, aliyekuwa Ofisa Mfawidhi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ukerewe. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Njalali na watu wengine watatu waliuwawa tarehe 23 Julai 2019, katika mapigano makali baina ya wananchi na Kikosi cha Doria cha Kuzuia Uvuvi Haramu, yaliyozuka kwenye Kisiwa cha Siza, Wilaya ya Ukerewe jijini Mwanza.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu, leo tarehe 26 Julai 2019, Jonathan Shanna, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza amesema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi, kuhusu tuhuma zinazowakabili.

Aidha, Kamanda Shanna amesema Jeshi la Polisi linawasaka watuhumiwa wengine, waliotoroka baada ya kutokea tukio hilo.

“Watu 7 wamekamatwa wanaendelea kuhojiwa kwa kina kuhusu tukio hilo. Baada ya tukio kutokea, wahalifu walikimbia kijiji. Tunaendelea kuwatafuta, ni vyema wakajisalimisha,” amesema Kamanda Shanna.

Wakati huo huo, Kamanda Shanna amesema mtu mmoja aliyejeruhiwa katika tukio hilo amepoteza maisha na kufikisha idadi ya watu watano waliopoteza maisha kutokana na tukio hilo.

Kamanda Shanna amesema mapigano hayo yaliibuka baada ya wananchi kutofautiana na maofisa wa kikosi cha Polisi cha doria cha kuzuia uvuvi haramu.

error: Content is protected !!