Saa 48 baada ya kuzikwa kwa Maalim Seif Sharif Hamad (77), aliyekuwa Makwamu wa Kwanza wa Rais, wa Serikali visiwani Zanzibar, Taifa likachukua mwelekeo mpya. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).
Mvumo wa mwelekeo mpya kuhusu virusi vya corona (COVID-19), ulianzia Zanzibar na baadaye kuiteka bara, lugha ya kufinyanga kuhusu uwepo wa virusi vya corona taratatibu ikaanza kubadilishwa.
Mlegezo wa kuzungumzia corona ulianza kwa Dk. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ilitoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na corona.
Taarifa ya wizara hiyo, ilitolewa baada ya saa 48 kupita, mwili wa Maalim Seif, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha siasa cha upinzani, ACT-Wazalendo, kuzikwa kijijini kwao Nyali, Mtambwe kisiwani Pemba.
Hiyo ilikuwa taarifa rasmi ya kwanza kutolewa na serikali ya Zanzibar na ile ya Tanzania hiyo kwa umma yenye lengo la kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Ni baada ya kufinyangwa kwa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo. Zanzibar kwa sasa haina Waziri wa Afya kwa kuwa Rais Hussein Mwinyi hajateua.
Kwa upande wa Bara, saa chache baada ya kifo cha Maalim Seif, kilichotokea saa 5:26 asubuhi ya tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, usiku wa siku hiyo saa 3:10, Rais John Magufuli, alitangaza kifo cha Balozi John Kujazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, kilichotokea Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.
Mabadiliko ya wazi kuhusu namna ya kujikinga na corona, yalidhihirishwa baada ya baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za serikali kuonekana hadharani wakiwa wamevaa barakoa.
Kwa Tanzania, ni kawaida kwa viongozi wa juu wa serikali kuonekana wakiwa hawajavaa barakoa, kuonekana kwa wachache kulileta picha tofauti ya uwajibikaji.
Rais wa zamani wa Tanzania katikati Dk. Jakaya Kikwete akiwa amevalia barakoa.
Siku moja baadaye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizungumza kwenye mazishi ya Balozi Kijazi yaliyofanyika Korogwe, Tanga kwamba hakuna kiongozi aliyekatazwa kuvaa barakoa.
Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson akapita njia hiyo, akihutubia waombolezaji kwenye msiba wa Dk Servacius Likwelile, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alisema, kutoonekana hadharani kwa viongozi wakiwa wamevaa barakoa, hakumaanishi kwamba wanamuogopa mtu.
Alisema, kila mtu anachukua tahadhari kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu na kwa kuzingatia hali yake ya kiafya. Akiwa na maana viongozi hao walikuwa wakichukua tahadhari kimya kimya.
Ndio wakati Dk. Tulia alikiri hadharani, kwamba aliwahi kuugua corona mara mbili, na hivyo hawezi kusema ugonjwa huo haupo. Kabla ya Maalim Seif kufariki, taarifa hizi hazikuwa zikitolewa.
Kabla ya kifo cha Maalim Seif, ilikuwa mwiko kuzungumzia uwepo wa virusi vya corona nchini, ilikuwa mwiko kwa waandishi, viongozi na madaktari. Sasa corona inaelezwa wazi na wananchi wanasisitizwa kuchukua tahadhari zote.
Leave a comment