July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rwanda yaikanyaga Tanzania kwenye utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu akibadilishana mawazo na wageni waliotembelea banda la Tanzania

Spread the love

UNAHITAJI kupitia hatua 26 kukamilisha utaratibu wa kufungua kampuni nchini Tanzania ili kuwekeza mradi wa kiuchumi utakaochangia nguvu katika kukuza pato la taifa.

Angalia tofauti: Burundi ni hatua tatu, Kenya kumi, Rwanda nane wakati Uganda ni hatua 15, karibu nusu ya zile za Tanzania.

Nini maana ya taarifa hii? Inamchukua mwenye fedha muda mfupi zaidi kujiongezea utajiri huku akichochea ukuaji wa uchumi kwenye nchi hizo, kuliko ilivyo kwa Tanzania. Matokeo yake?

Wawekezaji mahiri, wale wanaokerwa na ukiritimba au mlolongo wa hatua kabla ya kuanza kuwekezaji, wanakimbilia nchi hizo jirani, na kwa hivyo, kuchangia ukuaji wa uchumi wao kuliko nchi hii inayozizidi zote hizo kwa ukubwa wa eneo na idadi ya watu.

Pata haraka maudhui ya taarifa hii: Tanzania inazidi kuachwa kimaendeleo na jirani zake wanaoshirikiana katika mjumuiko wa Afrika Mashariki – The East African Community (EAC).

Tanzania ina bandari, maziwa, mlima mrefu zaidi barani Afrika, wa Kilimanjaro, mbuga za wanyama ikiwemo ya Selous na Serengeti zinazotambuliwa kama moja ya maajabu duniani, fukwe katika Bahari ya Hindi zenye mandhari ya kupendeza kwa vile hazijaharibiwa kimazingira, si kipaumbele cha matajiri duniani kama nchi inayofaa kwa uwekezaji miradi ya maendeleo ya kiuchumi – Foreign Direct Investment (FDI).

Wachumi wanaamini nchi kivutio cha miradi hii ndio yenye nafasi kubwa ya kukuza pato la taifa.

Tanzania ina hazina hiyo ya maliasili inayoonekana; huku chini ya ardhi ikiwa na mkururo wa madini kama dhahabu na tanzanite, yasiyopatikana kwingineko duniani.

Ni hazina ya kuvutia mitaji ya maelfu ya wawekezaji waadilifu kutoka mataifa yaliyoendelea, kwa upande mwingine ikiwa ndio kimbilio la watalii wa kiwango acha juu kutoka huko, wanaotaka sehemu tulivu ya kupumzika.

Kwa hivyo, biashara na uwekezaji vinakimbia nchi. Fedha inakosekana. Huko ni kujinyima nafasi ya kukuza uchumi wa Tanzania, nchi inayoendeshwa kwa mfumo wa muungano wa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar, jamhuri zilizoungana miaka 51 iliyopita.

Utalii ni sekta kuu ya kiuchumi Tanzania, ikitajwa kuchangia asilimia 17 kwa mwaka na hii ni kwa mujibu wa Prof. Benno Ndulu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa sababu ya utaratibu mbovu wa kumwezesha mwekezaji kufungua biashara, Tanzania imeshindwa kuingia katika nchi kumi bora zilizofana katika tamasha la kimataifa la utalii la Berlin, Ujerumani lililomalizika hivi karibuni.

Imepitwa na Kenya na Rwanda ambazo zimetokea juu ingawa zilikuwa na washiriki wachache, kulinganisha na Tanzania. Rwanda ilikuwa na washiriki wachache zaidi, imeibuka ya kwanza, ikifuatiwa na Kenya iliyoingiza chini ya kampuni 50.

Tanzania iliingiza kampuni 160, zikiwemo 60 za sekta binafsi, chini ya uratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), na kutokea kuwa iliyoongoza kwa washiriki wengi kuzidi nchi zote zilizoshiriki tamasha hilo kwa kanda ya Afrika.

Tamasha la safari hii lilishirikisha nchi 186 na kiasi cha watu 200 kutoka nchi mbalimbali duniani. Washindi huchaguliwa na kamati maalum ya majaji wapatao 30 ambao ni wataalam katika sekta ya utalii wanaotoka Chuo Kikuu cha Biashara cha Cologne (CBS).

Kamati hiyo hutembelea mabanda ya maonesho ya washiriki ana kuteua washindi kulingana na maeneo ya tathmini yaliyopangwa.

Rwanda iliibuka ya kwanza kimataifa na nafasi hiyo hiyo miongoni mwa nchi za Afrika. Kwa kundi la Afrika, Kenya imeibuka ya pili ikifuatiwa na Tunisia. Zilizofuata hapo ni Misri, Namibia, Ethiopia, Mauritius, Gambia, Seychelles na La Reunion.

Mkururo wa maofisa waandamizi kutoka serikalini ulishiriki tamasha hilo wakiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani – Deutsche Welle (DW) – siku ya kilele cha tamasha hilo mwishoni mwa wiki, Nyalandu alisema:

“Ushiriki mkubwa wa Tanzania ni matokeo ya kukua kwa sekta ya utalii nchini.”

Waziri Nyalandu amekuwa maarufu kwenye matamasha kama hayo tangu apandishwe wadhifa kuongoza wizara hiyo mapema mwaka jana.

Mwakilishi wa shirika la maendeleo la Japan (JICA), Onishi Yasunori akitambua tatizo sugu la nchi kutawaliwa na mfumo wa urasimu na hivyo kuvutia utoaji rushwa serikalini, anasema “haya kwa kawaida huvunja moyo wawekezaji na lazima serikali ichukue hatua kuyakomesha.”

Yasunori amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi kwamba ipo haja serikali kupunguza urasimu ili kujenga mazingira mazuri ya kibiashara. “Nimezungumza na wawekezaji wengi na wote wanataja tatizo hili la urasimu. Wengi wao wanasikitika mipango yao inakwama,” amesema.

Taarifa mbalimbali za utafiti nchini, zimethibitisha Tanzania inasumbuliwa na rushwa kiasi kwamba imeenea serikali kuu na katika Mahakama na Polisi, licha ya kuwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyobadilishwa na kupatiwa fedha nyingi za bajeti kila mwaka.

error: Content is protected !!