December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ruzuku yaendelea kushusha bei ya mafuta

Spread the love

 

MAMLAKA  ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini ambapo bei ya mafuta ya rejareja ya dizeli kwa Dar es Salaam na Tanga kwa Novemba 2022 imepungua kwa Sh 31 kwa lita na 34 kwa lita, mtawalia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 1 Novemba 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Modestus Lumato, ilieleza kuwa bei hizo zitakazoanza kutumika tarehe 2 Novemba, 2022 saa 6.00 usiku, zimeshuka ikilinganishwa na bei za Oktoba 2022 kwa sababu ya ruzuku.

Amesema bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kwa Bandari ya Dar es Salaam ingeongezeka kwa Sh 110,

“Hata hivyo, Serikali imetoa ruzuku ili bei iliyopo ya Oktoba 2022 isibadilike,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa upande wa Mtwara, Lumato amesema hakuna meli ambayo imehusishwa kwenye bei kwa Novemba 2022, hivyo, mabadiliko ya bei kwa Mtwara ni kwa ajili ya kuhusisha taarifa sahihi ya meli husika iliyotumika kwenye bei za Oktoba 2022.

Aidha bei ya mafuta ya taa na bei ya petroli kwa Tanga imepungua kwa Sh 164 kwa lita na Sh 118 kwa lita mtawalia ukilinganisha na bei zilizopita kwa kile alichoeleza kuwa ni wastani wa bei ndogo zaidi ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia na gharama za usafirisha kwa bandari ya Tanga.

Kutokana na ruzuku hizo bei katika mkoa wa Dar es Salaam imeendelea kubaki Sh 2,886 huku dizeli ikishuka kutoka Sh 3,083 hadi Sh 3,052 kwa lita. Mkoa wa Tanga bei ya petroli imeshuka kutoka Sh 2,924 Oktoba hadi Sh 2,806 kwa Novemba na dizeli ikishuka kutoka Sh 3,108 hadi Sh 3,074.

Kwa upande wa Mtwara bei imepanda kwa Sh 9 kwa petroli na kushuka kwa Sh 3 kwa dizeli na kufanya bei mpya ya petoli kuwa Sh 2,917 kutoka 2,908 na dizeli Sh 3096 kutoka 3,099.

error: Content is protected !!